AMA kweli
majanga yakimkuta binadamu hayapigi hodi! Daktari wa meno aliyejulikana
kwa jina la Dokta Ngariba (54), amejikuta ndani ya janga la tuhuma za
ngono baada ya wapiga picha wa Oparesheni Fichua Maovu (OFM) kunasa
sakata lake na mwanamke aliyedai ni mgonjwa wa jino aliyejitambulisha
kwa jina moja la Hamida (20).
Tukio hilo la kushangaza lilijiri Juni
9, mwaka huu ndani ya Kituo cha Afya cha Halmashauri ya Wilaya ya Temeke
kilichopo Kigamboni jijini Dar ambapo timbwili hilo lilitokea.
ILIKUWAJE?
Ilikuwa wakati OFM wakizunguka katika
Jiji la Dar es Salaam kama ada kusaka matukio ndipo walipopita nje ya
kituo hicho walisikia sekeseke kutokea kwenye chumba ambacho baadaye
kilibainika na cha kung’olea meno.
UCHUNGUZI, UFUATILIAJI
Katika uchunguzi na ufuatiliaji wa OFM,
mgonjwa huyo alisikika akidai kwa polisi waliofika kutuliza sakata kuwa,
alijihimu kwenye kituo hicho kwa lengo la kung’oa jino lakini katika
hali ambayo hakuitarajia daktari huyo alimtaka kimapenzi naye akajikuta
akitumbukia.
HEBU SIKIA HII
“Mimi nimekuja kung’oa jino, linaniuma
leo sijui siku ya ngapi? Lakini huyu daktari nimefika akanitaka
kimapenzi. Nilidhani anatania, baadaye nikagundua kuwa amedhamiria,”
alisema mwanamke huyo ambaye alikutwa ameshavua dera.
UTETEZI WA DAKTARI
Hata hivyo, daktari huyo hakumwacha
mgonjwa wake huyo atambe kiasi hicho, alijibu mapigo kwa kusema kuwa,
alimpokea mwanamke huyo kama mgonjwa wa jino na kumwingiza kwenye chumba
cha kung’olea meno lakini ghafla alimwona akianza kuvua nguo zake kisha
kumvua na yeye shati na baadaye kutaka kufungua zipu ya suruali.
Akiendelea kuzungumza mbele ya Polisi wa
Kituo cha Kigamboni waliofika kwenye sakata hilo ndani ya chumba cha
matibabu ya meno, daktari huyo alisema:
“Mimi sikuwa na nia mbaya, nilijua ni mgonjwa anataka tiba ya kung’olewa jino.
“Sasa nikiwa katika maandalizi ghafla
nikamwona anavua nguo na kisha akanivaa mimi na kuanza kunivua shati.
Nashangaa sana anaposema nilimtaka kimapenzi, si kweli jamani.”
MASWALI MAGUMU
Baada ya maelezo ya Dokta Ngariba, OFM ilikuwa na maswali yake lakini haikupewa nafasi ya kuyauliza kwa vile walidandia ishu.
Swali la kwanza; kama kweli Dokta
Ngariba alivamiwa na kuvuliwa nguo na mgonjwa huyo, alipiga kelele
kuomba msaada kutoka kwa watumishi wenzake?
Swali la pili; mpaka mgonjwa anajivua
nguo zake kisha kumvua yeye shati na baadaye kuelekea kwenye fraizi ya
suruali, yeye alikuwa anawaza nini akizingatia ni mgonjwa wa meno?
Uwazi lilizungumza na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sylvia Mamkwe kuhusu sakata hilo ambapo alisema:
“Taarifa hizo nazisikia kwako, niko
safarini, nitafuatilia. Kama ni kweli hatua zinachukuliwa kwa waajiri
wake ambapo najua kwa kosa kama hilo ni kupoteza kazi.”