MBALI na Askofu wa Kanisa la Full Gosple Bible
Fellowship, Zacharia Kakobe kuteswa na misukule inayodaiwa kufufuliwa na
baadhi ya makanisa ya kiroho nchini, Mchungaji wa Kanisa la Maombezi,
Anthony Lusekelo ‘Mzee wa Upako’ (pichani) naye ameibuka na kucharukia
suala hilohilo.
Akizungumza na Uwazi juzi, Mzee wa Upako alisema suala la misukule
linamtesa sana na kwamba anapingana na kufufuliwa kwao na baadhi ya
wachungaji wa makanisa mbalimbali wanaojigamba kufufua misukule wakati
si kweli na ni utapeli mtupu.
MZEE WA UPAKO ANAFUNGUKA:
“Kuna baadhi ya viongozi wa makanisa ya
kioroho (bila kutaja majina) wanadanganya watu kuwa wanatoa misukule,
si ukweli kabisa ni uongo. Wanatafuta namna ya kula sadaka za waumini
wao kwa kuonekana wanaweza sana mambo ya kiroho,” alisema Mzee wa Upako
na kuongeza:
“Hawa wachungaji wanatuchafua sana sisi tunaosimamia Neno la Mungu,
wanaharibu Kanisa la Mungu kwa kudanganya waumini wao kwa sababu ya pesa
tu. Hebu fikiria kuna wengine wanatoa hadi shilingi 400,000 kwa mtu
ili akubali kufanywa msukule feki na baadaye aombewe kanisani tena
nimesikia wanatengenezewa hati za kifo kuonesha kuwa kweli watu hao
walifariki dunia wakati si kweli, wamwogope Mungu.
“Huo ni usanii ndani ya Kanisa la Mungu. Nasema naumizwa sana na
wachungaji wa namna hii, nateseka sana na hili jambo. Ninayo mpaka CD za
mahubiri za baadhi ya viongozi wa makanisa wanaodanganya kuwafufua
misukule lakini kwa busara siwezi kuwataja ila wanajijua kwa sababu hata
dhamira zao zinawashuhudia.”
TURUDI KWA KAKOBE
Akikazia zaidi, Askofu Kakobe alisema, anayedai ana uwezo wa kufufua misukule ni muongo na kwamba atakuwa anaabudu shetani.
“Mwenye uwezo wa kufufua ni Yesu Kristo pekee na alifanya hivyo kwa
sababu ya utukufu wa Mungu na si vinginevyo, si binadamu wa kawaida
ambaye amepewa upako wa Mungu anadanganya watu kuwa anao uwezo wa
kumtoa mtu ambaye alichukuliwa msukule,” alisema Askofu Kakobe huku
akisisitiza kwamba mtumishi yeyote wa Mungu anaweza kufanya muujiza huo
kwa utukufu wa Mungu lakini si kwa sababu ya kuonesha yeye anaweza.