![]() |
| Emmanuel Okwi kulia akiwa na jezi ya Uganda, The Cranes. Je Micho atamuita kwa ajili ya mechi na Zambia? |
Thursday, 20 February 2014
FUFA WATAKA KUIVURUGIA YANGA KWA OKWI MECHI NA AL AHLY
YANGA
SC itacheza mechi ya marudiano na Al Ahly ya Misri mjini Cairo kati ya
Machi 7 na 9 katika Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya
mchezo wa kwanza Dar es Salaam Machi 1, mwaka huu.
Na
kikosini mwake ina wachezaji wawili tegemeo wa timu ya taifa ya Uganda,
The Cranes ambao ni washambuliaji Emmanuel Okwi na Hamisi Kiiza.
Uganda
imetangaza itacheza mechi ya kirafiki na Zambia, Chipolopolo iliyo
katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) Machi 5, mwaka
huu Uwanja wa Ndola, Zambia.
Hiyo
imethibitishwa na Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Soka Uganda (FUFA),
Edgar Watson baada ya kufikia makubaliano na wenzao, Chama cha Soka
Zambia (FAZ).
Kocha
Mserbia, Milutin Sredojevic ‘Micho’ bado hajataja kikosi ambacho
kitacheza na Zambia, lakini wakati wote amekuwa hawaachi Okwi na Kiiza
na bila shaka ataendelea na utamaduni huo.
Kama
Micho atawaita Kiiza na Okwi dhahiri ataathiri maandalizi ya Yanga kwa
ajili ya mchezo wa marudiano na Ahly, kwani watalazimika kwenda Uganda
mara tu baada ya mechi ya kwanza na mabingwa hao wa Afrika na kwa kuwa
watacheza mechi Ndola Machi 5, maana yake wanaweza kuondoka huko Machi 6
wakati tayari mabingwa wa Bara wakiwa Cairo.
Wakiitwa
Cranes, Okwi na Kiiza hawatapata fursa ya kushiriki mazoezi ya Yanga
kujiandaa na mchezo wa marudiano na Ahly, pia watachoka na safari na
mechi ngumu mfululizo.
Tanzania
pia itakuwa na mechi katika tarehe ya FIFA na kama kocha Mdenmark Kim
Poulsen ataita wachezaji wa Yanga kwa utaratibu wake wa kambi ya wiki
nzima kabla ya mechi, ina maana kambi ya maandalizi ya klabu hiyo
itapata pigo kubwa, kwa kuwa kwa sasa wachezaji wengi wa Stars hutokea
timu hiyo ya Jangwani.
Kitu
kizuri kwa Yanga SC na kusikia vikosi vya Uganda, Tanzania, Burundi na
Rwanda kwa ajili ya mechi za kirafiki za kimataifa mwezi ujao vinatajwa
bila ya wachezaji wao kujumuishwa. Mbali na Waganda Okwi na Kiiza, Yanga
ina Wanyarwanda Mbuyu Twite na Haruna Niyonzima kikosini.
