SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa), limetuma barua tatu tofauti
kwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, moja ikiwa ni ile inayomhusu
Emmanuel Okwi ambaye sasa yuko Yanga.
Moja ya barua ambazo Rage amepewa kopi na Fifa ni ile ambayo
Shirikisho la Soka la Uganda (Fufa), limemuomba Okwi kurejea Uganda na
kuitumikia timu ya taifa katika michuano ya kimataifa.
Pamoja na barua hiyo, Rage amethibitisha kupokea barua hizo tatu
kutoka Fifa ikiwemo ile ya Etoile du Sahel ya Tunisia kuomba kuongezewa
muda wa kulipa deni la dola 300,000 wanazodaiwa na Simba kutokana na
mauzo ya Okwi.
“Kweli nimepokea barua hizo, moja ni ile ambayo Etoile ambao mwezi
huu ndiyo ulikuwa mwisho kulipa dola 300,000, sasa wameomba waongezewe
muda hadi Septemba, mwaka huu ili waweze kulipa.
“Fifa wao
wamenitumia kopi lakini barua hiyo ni kutoka kwao Etoile kwenda Fifa na
wamethibitisha kwamba ni kweli Simba inawadai,” alisema Rage.
Barua ya tatu kati ya hizo kwa mujibu wa Rage ni ile ambayo
inaonyesha namna klabu hiyo ya Tunisia ilivyomshitaki Okwi kwa Fifa
kutokana na kuonyesha kukiuka mambo kadhaa wakati akijua mkataba wake
nao unamalizika mwaka 2016.
“Katika ile barua ya kuhusiana na suala la kulipa, Fifa wametaka
tusaini na kukubali kwamba sasa mwisho utakuwa Septemba 30 na tayari
barua hiyo nimeikabidhi kwa Hans Pope,” aliongeza Rage.
Tayari Okwi
yuko nchini na Yanga imemsajili ingawa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
limeamua kusimamisha usajili wake hadi litakapopata ufafanuzi kuhusiana
na usajili wake.
Wakati Fifa ilitoa kibali kwa Okwi kucheza SC Villa ya Uganda kwa
miezi sita, lakini Yanga ikamnunua na kuingia naye mkataba wa miaka
miwili, suala ambalo limezua mzozo mkubwa huku Simba wakiendelea
kusisitiza kulipwa fedha zao ambazo mwanzo walimuuza na hawakulipwa.
Okwi amekuwa akisisitiza kwamba anataka kuichezea Yanga ambayo
imemsajili, huku akieleza amekuwa akiumia moyoni kuona wenzake wakicheza
naye akiwa jukwaani kama mtazamaji.
