
Wakati
Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM ikimpitisha Godfrey Mgimwa (32)
kuwa mgombea wa chama hicho Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa, Kamati Kuu
ya Chadema inakutana keshokutwa kuteua jina la mgombea wake.
Mgimwa ni
mtoto aliyekuwa Mbunge wa Kalenga na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa
aliyefariki Januari Mosi mwaka huu, Afrika Kusini alikokuwa akipata
matibabu.
Katibu wa
Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nauye alisema jana
kuwa jina hilo lilipitishwa kwenye kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika
Ikulu chini ya Mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete.
"Kwa hiyo tunatangaza rasmi kwamba Godrey Mgimwa ndiye mgombea wa chama chetu Jimbo la Kalenga," alisema Nape.
Kabla Kamati
Kuu haijampitisha, Mgimwa wiki iliyopita alishinda kura za maoni kwa
kupata 342, huku mshindi wa pili Jackson Kiswaga akipata kura 170,
watatu ni Hafsa Mtasiwa aliyeambulia kura 42
Tayari Tume ya Uchaguzi imepanga Machi 16, mwaka huu kuwa siku ya uchaguzi Jimbo la Kalenga.
huku kampeni zikifanyika kuanzia Februari 19 hadi Machi 15.
Akifafanua, Nape alisema wana CCM wana imani na mgombea huyo kuwa atashinda kwa kishindo na kulichukua jimbo hilo.
Naye Ofisa
habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema mbali na CC kufanya uteuzi,
pia itapokea ya uchaguzi wa madiwani uliofanyika mwishoni mwa wiki.
Makene
alisema pia kuwa Kanda mbalimbali kulikofanyika uchaguzi huo, zilipewa
jukumu moja la kuhakikisha mambo yanakwenda vema, lakini kutokana na
matokeo yaliyopatikana, kila Kanda inatakiwa kuandika ripoti ya uchaguzi
huo kabla ya CC kutoa kauli rasmi ya kufanyika uchaguzi huo.
Nape ajibu hoja
Akijibu
shutuma kwamba, jimbo hilo linarithishwa kifamilia, Nape alisema chama
hicho hakiwezi kumnyima mwanachama yeyote haki ya kuwania kwa sababu tu
wazazi wake waliwahi kuwa viongozi.
"CCM haiwezi
kumzuia Godfey kuwania eti kwa sababu ni mtoto wa marehemu Dk Mgimwa,
yeye ana haki ya kuwania kama watu wengine tunachoangalia ni uwezo wake
na hilo limeonyeshwa baada ya wananchi wa Kalenga kumpa ushindi wa
kishindo," alisema.
Alivionya
vyama vya upinzani kwamba muda wa kampeni ukifika kufanya mikutano ya
kistaarabu kwa sababu chama hicho hakitavumilia vurugu.
Aliwapiga
kijembe Chadema kuwa wanatakiwa kuandaa Chopa nyingi zaidi ili ziweze
kuwazungusha katika kata 13 ilizopo kwenye Jimbo hilo ili wajaribu
bahati yao.
Naye Mgimwa akizungumza, aliishukuru Kamati Kuu kwa kumpitisha kuwa mgombea ubunge katika jimbo hilo.
"Natoa
shukurani zangu za dhati kwa Kamati Kuu kunipitisha kugombea ubunge,
sitawaangusha," alisema Mgimwa ambaye anafanya kazi katika Benki ya
Stanbic.
Kamati Kuu
jana jioni iliendelea na kikao chake ikiwa ni maandalizi ya Kikao cha
Kamati ya Maadili kitakachokaa kesho mjini Dodoma.
Kikao hicho
kinatarajia kuwahoji baadhi ya vigogo wa chama hicho waliokiuka maadili
ikiwemo kutangaza kugombea urais kinyume na taratibu za chama hicho.