KLABU ya Azam FC ya Dar es Salaam imefungwa mabao 2-0 na wenyeji Ferroviario Beira kwenye Uwanja wa Ferroviario Beira mjini Beira Msumbiji katika mchezo wa marudiano, Raundi ya Awali, Kombe la Shirikisho Afrika jioni hii.
Katika mchezo huo, uliofanyika sambamba na mvua kali iliyoharibu mandhari ya Uwanja, wenyeji walipata bao moja kila kipindi.
Mabao hayo yote ya Ferroviario Beira yamefungwa na mshambuliaji wake hatari, Mario Simamunda dakika ya tano na ya 70.
Wachezaji wa Azam FC kutoka kulia beki Aggrey Morris, Kipre Tchetche na Brian Umony. |
Matokeo hayo yanaifanya Azam itolewe kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya awali kushinda bao 1-0 mjini Dar es Salaam, bao pekee la mshambuliaji Kipre Herman Tchetche Uwanja wa Azam Complex, Chamazi
.
Aidha, matokeo hayo pia yanamaanisha, Azam imeshindwa kufikia rekodi yake ya mwaka jana katika michuano hiyo, ilipotinga hatua ya 16 Bora na kutolewa na AS FAR Rabat ya Morocco chini ya kocha Muingereza, Stewart John Hall, aliyejiuzulu Septemba mwaka jana.
Matokeo hayo pia, yanamaanisha kocha Mcameroon Joseph Marius Omog ameshindwa kuendeleza rekodi yake nzuri aliyotoka nayo Kongo Brazaville, akiiwezesha Leopard FC kutwaa Kombe la Shirikisho.