Awali,
Yanga ilitangaza kuwa itamtumia Okwi katika mechi hiyo licha ya kuzuiwa
na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), kwa kile kilichoelezwa ni
kutokamilika kwa kesi zake tatu zilizopo Shirikisho la Soka la Kimataifa
(Fifa), lakini mpaka kufikia jana hali ya mambo ilikuwa tata.Licha ya kutoa kauli hiyo kupitia kwa Katibu wao Mkuu, Beno Njovu, wiki iliyopita, uongozi wa Yanga ulikuwa ukiendelea kuhaha kwenye ofisi za TFF kuhakikisha Okwi anapata kibali cha kucheza katika mechi hiyo kwa kuwa walidai Okwi amezuiwa na TFF kwa madai yanayoihusu Fifa na siyo Shirikisho la Soka la Afrika (Caf).
Jana majira ya saa tisa alasiri, Championi Ijumaa lilipomtafuta Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, wote walisema kuwa wapo kwenye kikao bila kufafanua ni cha nini.
Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alipoulizwa alisema bado hawajapata leseni ya mchezaji huyo kutoka Caf, ambalo ndilo linalosimamia michuano hiyo. “Hatujapata taarifa yoyote kutoka TFF kama Caf imetuma leseni ya Okwi, hivyo tunaendelea kusubiri,” alisema Kizuguto.
Aidha, saa 11 jioni, alipotafutwa Wambura alisema: “Leseni za wachezaji wa Yanga kutoka Caf zimeshafika.” Kuhusu leseni ya Okwi alisema: “Hilo unatakiwa kuwauliza Yanga ndiyo wenye mchezaji.”
Alipoafutwa Kizuguto baada ya majibu hayo ya Wambura, alisema: “Hatujaziona hizo leseni, wao TFF ndiyo wanatakiwa kuweka wazi na siyo kufichaficha suala hilo.”
Hata hivyo wakati tunaingia mtamboni, taarifa za uhakika zilieleza kuwa leseni zilizoletwa ni 25 wakati
Yanga ilituma majina ya kuomba lesi kwa wachezaji 26.
Okwi ambaye hajacheza mechi zote tatu za Ligi Kuu Bara kutokana na kesi hizo, alikuwa kambini Bagamoyo na kikosi cha timu hiyo kilichokuwa kikijiandaa kwa ajili ya mchezo huo.
