Monday, 16 December 2013
PICHA YA MANDELA AKIWA KWENYE JENEZA YAWA DILI
Na Mwandishi Wetu
HATIMAYE historia imeandikwa, Mzee Nelson Mandela, rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini amezikwa jana katika shughuli kubwa iliyoshuhudiwa na mamilioni ya watu duniani kote kupitia runinga huku picha ya mwili wake ukiwa ndani ya jeneza ikiwa ndiyo dili kubwa.
Mazishi ya Mzee Madiba aliyefariki dunia Desemba 5, 2013 yalifanyika katika kijiji alichokulia, Qunu, Mkoa wa Mthatha katika Jimbo la Eastern Cape nchini humo.
Wiki iliyopita, serikali ya Afrika Kusini ilitoa amri kwamba haruhusiwi mtu yeyote kupiga picha ya mwili wa marehemu akiwa anaagwa jijini Pretoria.
Familia nayo ikapigilia msumari wa mwisho ikisisitiza kuwa, binadamu yeyote mwenye akili timamu haruhusiwi kupiga picha ya mwili huo ukiwa ndani ya jeneza.
Amri hiyo ilivivunja nguvu vyombo mbalimbali vya habari duniani ambavyo vilikuwa nchini humo vikifuatilia mazishi na maziko ya Mandela.
Serikali iliweka wazi kwamba, mtu yeyote atakayepiga picha, akinaswa zitafutwa kwanza halafu kama ni Msauzi atashitakiwa na kama ni raia wa nje atarudishwa nchini mwake na kupigwa marufuku kuingia nchini humo maishani mwake.
Baadhi ya watu nchini humo wamekuwa wakihaha kupata picha hiyo ili waitengenezee fremu na kuiingiza sokoni kwa wanunuzi.
Juzi, baadhi ya mitandao iliweka sehemu ya sura ya Mandela na kudai ni picha yake akiwa kwenye jeneza siku chache baada ya kifo.
Hata hivyo, haraka sana, baadhi ya vyombo vya usalama nchini humo vilikanusha na kusema picha hiyo ni enzi za uhai wake akiwa amelala.
Ukawekwa ushahidi wa picha hiyo ikiwa yote ambapo Mzee Madiba alikuwa akiuchapa usingizi wakati fulani enzi za uhai wake.
Kuhusu maziko yake, zaidi ya wageni 4,500 kutoka pande zote za dunia walihudhuria ndani ya hema kubwa lililojengwa katika eneo la familia ya Mandela huku mamia ya wanakijiji na baadhi ya wanafamilia wakikosa nafasi ya kuuaga mwili wa mpendwa wao huyo.
Idadi kubwa ya viongozi waliohudhuria, wakiwemo Rais Barak Obama wa Marekani na mtoto mkubwa wa Malkia wa Uingereza, Prince Charles, kumelifanya eneo la kijiji hicho kuwa dogo na linalohitaji uangalizi wa hali ya juu wa usalama. Katika kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa kiusalama, ndege mbili za jeshi la nchi hiyo zilikuwa angani pamoja na helikopta kadhaa.
Zaidi ya wanajeshi 20,000 walilinda usalama katika kijiji hicho wakifanya kazi sambamba na jeshi la polisi.
Licha ya wenyeji na majirani hao wa marehemu Mandela kunyimwa fursa ya kuuaga mwili huo, pia walizuiwa kuukaribia kutokana na uhaba wa nafasi, kitendo ambacho kililalamikiwa sana.
Waliokosa nafasi ya kuhudhuria mazishi hayo siyo tu majirani, bali hata mtoto wa kaka mkubwa wa Mandela, Maurice aitwaye Mzwandile Mandela mwenye umri wa miaka 13.
Mwingine ni mpwa wa Mandela, Gloria Mkwedini, mtoto wa dada yake ambaye pia hakuhudhuria mazishi hayo pamoja na familia yake ya watu 16.
Watu hao wanaishi maili chache kutoka kwa Madiba wakiwa wanaishi katika moja ya nyumba nyingi za mduara zilizoko katika eneo hilo.
Na kwa vile hakuna umeme, hawakuweza kufuatilia tukio hilo katika televisheni.
‘Hii imetufanya tujione kama ni watu wageni tuliotengwa,” alisema Gloria akimlaumu mtoto mkubwa wa kike wa Mandela, Makaziwe, 59, aliyedai kuwa ndiye aliyekuwa anaamua nani aalikwe na nani aachwe.
Alisema mume wake alimfuata Makaziwe na kutaka kupewa mwaliko, lakini binti huyo alikataa. Alilalamika kuwa kunyimwa kwao mwaliko kunatokana na umasikini wao.
Mandela alizikwa kimila, kwa ndugu wa karibu wa familia yake pamoja na viongozi wa kimila wapatao 70 waliokabidhiwa mwili huo na kuuingiza ndani ya nyumba yake ya milele huku pia wakikataa tukio hilo kurushwa na chombo chochote cha habari.
Miongoni mwa mila na desturi za kabila la Mandela linalofahamika kwa jina la Aba Thembu ni pamoja na kuchinjwa kwa ng’ombe dume aliyenona na damu yake kumwagiwa ndani ya kaburi la marehemu.
Taifa la Afrika Kusini limekuwa lenye pilikapilika nyingi tangu kufariki dunia kwa mpigania haki huyo Desemba 5, mwaka huu, nyumbani kwake jijini Johannesburg baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa mapafu.
Mwili wake uliondolewa saa tisa usiku na kupelekwa katika hospitali ya kijeshi jijini Pretoria ambako kwa siku tatu kuanzia Jumatano, uliwekwa katika majengo ya Ikulu ambako zaidi ya watu laki moja waliripotiwa kuuaga.
Hata hivyo, serikali ilitoa amri ya kusitishwa kwa shughuli hiyo huku maelfu ya wananchi wakiwa katika msururu mrefu wakisubiri kupata nafasi ya kumuaga mtu anayedhaniwa kuwa ndiye maarufu na mwenye heshima zaidi kuliko wote katika karne ya 21.
CREDIT: GPL