Tuesday, 17 December 2013

MAWAZIRI MIZIGO ISICHUKULIWE KISIASA

NIANZE kwa kumshukuru sana Mungu kwa kutuwezesha kuifikia siku ya leo tukiwa salama salimini. Kama ninavyosema siku zote, ni muhimu sana kumkumbuka na kumsifu muumba kwa sababu sisi tumepata bahati ya kuifikia leo siyo kwa ujanja tulionao, bali kwa rehema zake pekee.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Moses Nnauye.
Wakati Afrika yote ikiwa bado na simanzi kwa kifo cha shujaa wetu, mzee Nelson Mandela aliyezikwa juzi, hapa nyumbani habari kubwa hivi sasa ni kuhusu kujieleza kwa mawaziri kadhaa mbele ya kikao cha Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mawaziri hao wanatakiwa kujieleza kwa kile kinachodaiwa kushindwa kutimiza majukumu yao, kama Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana alivyopata kunukuliwa akisema, kuwa baadhi ya watendaji wa serikali, wakiwemo mawaziri hawawajibiki ipasavyo.
Hivi sasa kuna msemo ambao umekuwa maarufu mitaani kama mawaziri mizigo. Ni lugha inayoweza kukupa picha ya kejehi ambayo wanapewa viongozi hao.
Binafsi nimeliangalia suala hili kwa umakini na kugundua kuwa CCM ilichelewa sana kuchukua hatua kama hii ili kusimamia vizuri uwajibikaji wa viongozi katika utendaji wao wa kazi.
Sisemi hivi kwa kuwazungumzia mawaziri hawa walioitwa, isipokuwa najaribu kupongeza utaratibu huu kwa vile ungesaidia sana kuwafanya watendaji wetu kuwa na hofu na kazi zao.
Na suala hili lisiwe la watendaji wanaodhaniwa kutotimiza majukumu yao vyema, bali liwe ni la kudumu kwa kila kiongozi kutakiwa kueleza mbele ya Kamati Kuu jinsi gani alivyoshiriki katika kutekeleza ilani ya chama.
Wananchi wanailaumu CCM kutokana na kutoridhishwa na utendaji wa watendaji wa serikali, ambao wanajifanyia kana kwamba hawana mtu wa kuwauliza na kuwawajibisha. Kama utaratibu wa kujieleza mbele ya kikao kikubwa kama hiki utafanywa, ni wazi kuwa viongozi wetu wangejikuta wakipata hofu na hivyo kujitahidi ili wapate kitu cha kusema mbele ya vikao.
Utaratibu huu unafaa kufanywa siyo kwa mawaziri tu, bali hata watendaji wa taasisi zingine kubwa za serikali kama Shirika la Nyumba, NSSF, PPF, BOT, Air Tanzania, Bandari, Reli na mengineyo.
Hii ni kwa sababu wakubwa wetu katika ofisi za umma wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea, ndiyo maana matatizo ya watanzania yanazidi kuongezeka kila siku badala ya kupungua kutokana na ukosefu wa uwajibikaji na hata ubunifu.
Haiwezekani Tanzania iendelee kuwa na matatizo yale yale kila mwaka wakati serikali inatenga fedha na watu wa kusimamia wanateuliwa, lakini bila mabadiliko. Ipo haja kwa Kamati Kuu ya chama kukifanya kitendo hiki kuwa endelevu kwa vile wao ndiyo watakaokuja kupata wakati mgumu kipindi cha uchaguzi kwa vile wataonekana kushindwa kutekeleza ahadi zao.
Cheo ni dhamana, siyo kitu cha mtu wala hisani. Kama mtu amepewa nafasi hiyo, anapaswa kuifanya kwa kiwango kikubwa ili kukidhi matarajio ya wananchi kwa sababu kwao kila siku hali inazidi kuwa mbaya.
Ni jambo la kushangaza kuona kwamba tunalo Baraza la Mawaziri ambalo lina watu wanaoonekana kama ndiyo wanafanya kazi kubwa ya kuwatumikia wananchi kuliko wengine. Kwa watu wanaofanya kazi kama timu, kutokea kwa kitu hiki ni aibu.
Kwa nini mtu mmoja aonekane anafanya kazi nzuri na mwingine aonekane ni mzigo? Jibu la swali hili ni moja tu, kwamba wapo ambao hawana nia ya dhati ya kumsaidia Rais isipokuwa wapo pale kwa ajili ya masilahi yao binafsi.
Mbona kuna baadhi ya mawaziri wamekuwa wakifanya vizuri karibu kila wizara wanayopelekwa wakati wengine kila wanapopelekwa wanaboronga?
Ndiyo maana nimejiridhisha kwamba ni vyema utaratibu huu ungekuwa wa kudumu badala ya kuwa wa zima moto. Siyo mpaka viongozi wa chama waende vijijini wakutane na madudu ndipo waibuke na kutaka Kamati Kuu iwaite wahusika na kuwahoji.
Hili liwe ni jambo la kawaida katika utendaji kazi wa chama kwamba kitakutana na mawaziri wanaoundwa na serikali yake ili ipate majibu ya utekelezaji wa ilani ya chama, kama ilivyojinadi mbele ya wapiga kura.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.