Tuesday, 17 December 2013

Bomu Arusha: Lema aishukia Kamati ya Bunge


  Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema akichangia mjadala bungeni wa Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama Mjini Dodoma jana.


Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ameeleza kushangazwa na hatua ya kamati ya Bunge kukwepa kuzungumzia suala la kurushwa bomu kwenye mkutano wa chama chake huko Arusha, Julai 15, mwaka huu.
Akichangia mjadala wa taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Ulinzi na ya Mambo ya Nje, bungeni jana, Lema alisema kamati hizo ziligusia suala la bomu lililorushwa kwenye Kanisa Katoliki Olasiti, Arusha na kuachana kuzungumzia lile la mkutano wa Chadema uliofanyika kwenye Viwanja vya Soweto.
Alisisitiza msimamo wa Chadema kuwa kinao mkanda wa video unaoonyesha mtu aliyelipua bomu Uwanja wa Soweto na kushangaa taarifa ya kamati hizo mbili kutokuzungumzia tukio hilo.
Alisema ushahidi huo ungewezesha vyombo vya ulinzi na usalama kumbaini mtu aliyerusha bomu hilo na kusisitiza kuwa wako tayari kukabidhi mkanda huo kwa tume huru itakayoundwa na Serikali kuchunguza tukio hilo.
“Lakini bahati mbaya alikamatwa jambazi kule Nzega akapigwa ili anitaje mimi ndiye niliyerusha bomu Olasiti na nilipigiwa simu na mmoja wa ndugu wa jambazi huyo akaniambia kuhusu suala hilo... Tunao ushahidi nani alitaka kutuua, Serikali iunde tume tupeleke ushahidi wetu,” alisema.
Bomu katika uwanja huo lililipuka wakati Chadema kikihitimisha kampeni zake za udiwani katika Kata ya Kaloleni.
Mei 5, mwaka huu, watu wasiojulikana walirusha bomu katika mkusanyiko wa kidini katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti na kusababisha vifo vya watu watatu.
...Amshukia Ole Medeye
Lema pia alimtuhumu Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye kwa madai ya kula njama kuwapa sumu watu ambao si wenyeji wa Mkoa wa Arusha.
Alisema ana mkanda wa video (DvD) ukimwonyesha naibu waziri huyo akitoa maelekezo ya kupigwa mishale na mikuki kwa watu wasio wenyeji wa Mkoa wa Arusha.
Hata hivyo, Ole Medeye alipoulizwa jana kuhusu tuhuma hizo alimtaka Lema ampatie mkanda huo ili autazame kujiridhisha kabla ya na kutoa majibu yake kupitia bungeni.
Naibu Waziri huyo alisema aliapa kuilinda Katiba ya nchi inayotoa uhuru wa mtu kuishi mahali popote bila kubaguliwa kwa jambo lolote hivyo atakuwa mtu wa mwisho kutoa kauli za aina hiyo.

“Najua siku hizi zipo DvD za kutengeneza, kuna utaalamu wa kuzibaini kwa hiyo sina shaka yoyote,” alisema Ole Medeye.
Medeye ambaye pia ni Mbunge wa Arumeru Magharibi (CCM), alisema Lema yuko katika wakati mgumu kisiasa na kauli aliyoitoa ni ya mfa maji ambaye anakaribia kufa hivyo hutapatapa akitafuta mtu wa kufa naye.
Akichangia taarifa za kamati hizo mbili, Lema alitumia fursa hiyo kuhoji kwa nini Ole Medeye aliyehudhuria kikao cha kuchochea ukabila asitajwe kama mtu mhalifu wa kwanza duniani.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo DVD ya Naibu Waziri wa Ardhi akiwa kwenye kikao cha ukabila wakati wa uchaguzi katika kampeni za udiwani Arusha Mjini na kutoa maazimio ya kuwapa wageni sumu na kuwapiga mishale na mikuki,” alisema.
Alisema katika kikao hicho ambacho alidai Ole Medeye ndiye aliyekisimamia, pia kulitolewa maazimio ya kuhakikisha wageni hawauziwi mashamba.
“Taarifa hizo nilipeleka polisi, pia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, OCD (Kamanda wa Polisi wa Wilaya) na John Mongela (Mkuu wa Wilaya wa Arusha), ambaye nilimwambia na alikiri amelisikia na analifanyia kazi suala hilo lakini mpaka leo hakuna lolote....
“Naibu Waziri anakaa kwenye kikao na kuhamasisha ukabila kwa sababu tu chama chake kishinde uchaguzi. Mheshimiwa Mwenyekiti taifa hili litakwenda mahali pabaya sana.”
Lema alisema wanaochochea siasa ya udini na ukabila siyo Waislamu na Wakristo walioko misikitini na kanisani, bali ni wanasiasa wanaotafuta nafasi za kuongoza kama alivyofanya Ole Medeye katika kampeni hizo.

credit mwananchi