WATOTO wawili wa familia moja, Nuru (3) na Dora
Kaitaba (2), wamefariki dunia kwa kuungua moto hadi kubaki majivu baada
ya moto mkubwa uliotokana na petroli kulipuka nyumbani kwao, Mapinga,
Bagamoyo mkoani Pwani.
Tukio hilo lililowaliza wengi, lilijiri saa tatu usiku, Jumapili iliyopita watoto hao wakiwa ndani na baba yao.
Kwa mujibu wa mashuhuda, baba mzazi wa watoto hao, Kaitaba ambaye ni
mpiga picha wa kujitegemea, alikuwa amerejea kutoka Bunju B alikofuata
petroli ambayo huiuza katika vipimo vidogo vya kwenye makopo ya maji
nyumbani hapo.
Ilizidi kudaiwa kuwa alipofika kwake alishusha mzigo wa mafuta,
watoto wake hao walikuwa wamelala katika kibanda chake cha biashara.
Ghafla, mashuhuda wanasema, umeme ulikatika hali iliyomfanya Kaitaba
kuchukua mshumaa na kuuwasha ili andelee na shughuli zake za kuhudumia
wateja.
“Baada ya kuwasha mshumaa, moto huo ulidakwa na petroli hiyo iliyokuwa kwenye dumu na kusababisha mlipuko mkubwa.
Mashuhuda walisema Kaitaba alikimbia kutoka bandani, lakini alipopata
akili ya kuwaokoa watoto wake tayari moto ulishakuwa mkubwa na hivyo
kumfanya apige kelele za kuomba msaada.
Hata hivyo, majirani walishindwa kuingia ndani kutokana na ukubwa wa moto huo na uduni wa vifaa vya kuzimia.
Watu wakiwa wanaangalia tukio hilo kwa masikitiko makubwa, Kikosi cha
Zimamoto Bagamoyo kiliwasili kikiwa kimechelewa hivyo kuambulia kuchukua
majivu ya watoto hao wawili waliaochana mwaka mmoja kuzaliwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, SACP Onesphory Matei
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema tofauti na madai ya
baadhi ya watu kuwa baba mzazi wa watoto hao anashikiliwa na polisi,
alichukuliwa na kupelekwa hospitali kwa ajili ya kutibiwa majeraha na
hatachukuliwa hatua yoyote kwa vile kilichotokea ni ajali.
Aidha
Kamanda Matei alitumia fursa hiyo kupiga marufuku biashara hiyo ya
mafuta ya petroli na dizeli ambayo ni maarufu wilayani humo.
Marehemu walizikwa Jumatatu iliyopita kwenye Makaburi ya Bunju, Kinondoni, Dar.
Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi, Amina.