TABIA ya staa wa filamu za Kibongo, Jacqueline
Wolper kubadilibadili dini mara kwa mara imeonekana kuwakera watu
mbalimbali akiwemo Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum
ambaye amemcharukia vikali.
Wolper kiimani ni Mkristo lakini hivi karibuni alibadili na kuwa
Muislam kabla ya kurejea tena kwenye imani yake ya awali ya ukristo.
Sababu ya Wolper kubadili dini ilikuwa ni kufunga ndoa na aliyekuwa
mchumba wake Abdallah Mtoro ‘Dalas’, walipoachana akaamua kurudi kwenye
ukristo.
Akizungumza na Risasi Jumamosi juzikati, Shehe Salum, alisema Wolper
anapaswa kujichunguza na kubadilika haraka kwani kitendo anachofanya ni
kinyume na taratibu za dini.
“Siyo vizuri hata kidogo na hata dini zote zinakemea kitendo cha kuchezeachezea dini kwani ni chukizo kwa Mungu.
“Kwa upande wa Dini ya Kiislamu, kuna sheria kali zaidi kwa mtu
akionekana na tabia hiyo, anaweza hata kuuawa hivyo wanaofanya mchezo
huo waache kwani siyo vizuri. Huko ni kumfanyia Mungu dhihaka,” alisema
Shehe Salum na kuongeza:
“Unajua suala la imani ni kitu kinachomhusu mtu binafsi, ni vyema
kufanya uamuzi wa hakika na kushika njia moja na siyo kufanya dhihaka na
dini ya Mwenyezi Mungu. Ni kitu kibaya sana.”
Naye Juma Suleiman,
mkazi wa Ilala, jijini Dar es Salaam alimwambia mwandishi wetu kuwa,
katika imani ya kiislam kunakatazwa watu kucheza na dini huku
akisisitiza anayefanya hivyo anaweza kulaaniwa.
“Dini siyo kitu cha kuchezea, ni daraja la kumfikisha mtu kwenye
haki, si mahala pa kuingia na kutoka, kuingia na kutoka. Huko ni kucheza
na Mungu. Namshauri huyo mtoto (akimaanisha Wolper) abadilike. Asifanye
mchezo na imani, Mungu anaweza kumlaani kwa kumchezea,” alisema
Suleiman.