Kijana
Amos Ng’arare Sasi mwenye umri wa miaka 21, mkazi wa Kijiji cha Kizaru,
Kata ya Mryaza, Musoma vijijni anyesumbuliwa na uvimbe.
Ni mateso makubwa.
Kwa karibu miaka 17 sasa, kijana Amos
Ng’arare Sasi mwenye umri wa miaka 21, mkazi wa Kijiji cha Kizaru, Kata
ya Mryaza, Musoma vijijni anataabika kwa ugonjwa ambao umempeleka katika
hospitali nyingi bila mafanikio.
Kama angeendelea na masomo yake vizuri,
hivi sasa Amosi angekuwa kidato cha nne, lakini alilazimika kukaa
nyumbani na kuwaacha wenzake wakiendelea na masomo katika Shule ya
Sekondari ya Bumangi kutokana na uvimbe kuzidi kukua.
Kwa sasa yupo katika Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili anakotibiwa. Akizungumza na mwandishi wa habari hii alikuwa
na mengi ya kusimulia:
“Ninaumia sana moyoni niwaonapo
wanafunzi wenzangu niliosoma nao darasa moja wakiendelea na masomo
wakati miye nakabiliana na gonjwa hili la ajabu ambalo limezima ndoto
zangu juu ya elimu, sitegemei kurudi tena darasani, nilizaliwa nikiwa
sina tatizo kiafya, nililelewa na wazazi wangu wote wawili, nikawa
naishi vizuri kama watoto wenzangu.
“Tatizo lilianza kama kaupele hivi
nikiwa na umri wa miaka minne, kidogo kidogo kikawa kinakua, lakini
bahati mbaya baba alifariki na mama akabeba mzigo wa kunihudumia kwa
matibabu, licha ya kipato chake kidogo kwani alitegemea kilimo, tena cha
jembe la mkono.
“Pamoja na mama kunipeleka hospitali
mbalimbali, nilikuwa napewa asprini tu kwa ajili ya kutuliza maumivu
kwani walishindwa kunipa dawa za aina nyingine kutokana na ugonjwa wangu
kutofahamika.
“Mama anahangaika na mimi hadi namuonea
huruma, kaka yangu mkubwa alitoweka nyumbani tangu mwaka 1998 akisema
anaenda kutafuta kazi, mpaka sasa hajulikani alipo na wala hajawahi
kurudi nyumbani, hali ilizidi kuwa mbaya nilipofikisha umri wa miaka
tisa, maumivu na uvimbe ukazidi.
“Mama alikuwa hapati usingizi aliponiona
nahangaika, alinipeleka hospitali ya Musoma haikusaidia, mwaka 2010
nilipelekwa Bugando kufanyiwa uchunguzi, ugonjwa haukujulikana, wakati
huo ndiyo nilikuwa nikianza kidato cha kwanza, nilienda siku chache.
“Nilirudishwa nyumbani, baadhi ya watu
wakawa hawataki kuniona mitaani, wakaniona kama vile nimeleta nuksi
katika ukoo, nikawa najificha ndani.
“Baadhi ya wananchi walinionea huruma
walinichangishia fedha ili nije Muhimbili, mara ya kwanza nilifika hapa
Septemba 2011, nikachukuliwa vipimo na kuambiwa nirudi nyumbani hadi
Desemba.
“Hata hivyo, sikuweza kurudi kipindi
hicho kutokana na kukosa nauli, baadaye nikafanikiwa kwenda nyumbani.
Tatizo likawa namna ya kufuata majibu, lakini baadaye nilipata.
“Mara ya pili nilikuja Februari mwaka
huu kwa msaada wa nauli kutoka kwa diwani wetu pamoja na Mbunge Nimrodi
Mkono, walinipima kwa mara ya pili na kunieleza kuwa kuna mshipa wa
fahamu unapitisha damu nyingi hivyo natakiwa kufanyiwa upasuaji nchini
India.