HAKUNA neno zuri la kusema zaidi ya Mungu mkubwa!
Ule mtafaruku ndani ya ndoa ya mwimba Injili mahiri Bongo, Flora na
mumewe, Emmanuel Mbasha umedaiwa kumalizika kwa wawili hao kupatana,
Risasi Jumamosi linakuwa nambari wani kukuhabarisha.
Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika, wawili hao walikalishwa kikao cha upatanishi mapema wiki hii kilichokuwa chini ya familia.
MANENO YA CHANZO
“Kikao cha familia kilikaa, Mbasha aliitwa
akafika, Flora naye aliitwa akatokea, mazungumzo yalikuwa marefu lakini
kimsingi waliamua kuweka kando mtafaruku wao na kuijenga upya ndoa yao,”
kilisema chanzo.
Chanzo kiliongeza kuwa katika kikao hicho cha mwanzoni mwa wiki hii,
miongoni mwa adidu za rejea ilikuwa kutokumbushia vikao vilivyopita
ambapo hakukupatikana muafaka.
VIKAO VILIVYOPITA
Katika vikao vilivyopita, wahusika wakuu
walikuwa wazazi wa Mbasha (mzee Maneno Mbasha, Zulfa Maneno), ndugu wa
Flora na Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
VIKAO VYA BAADAYE
Kwa mujibu wa chanzo, vikao vilivyofuata,
wawili hao wakawa tayari kila mmoja ametema nyongo yake pembeni na
kufikia makubaliano kwamba, ndoa yao isimame tena wakitumia maandiko
kwenye Biblia kutoka kitabu cha Waebrania yanayosema: Ndoa na
iheshimiwe na watu wote na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na
wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.
WAKORINTHO YAFUNGA KAZI
Kwa mujibu wa chanzo hicho, maneno
mengine ya Biblia yaliyotumika kwenye kikao hicho mpaka wawili hao
wakaamua kurudiana ni 1 Wakorintho 7:1-10 ambapo maandiko yanasema:
Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe na
kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake
vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake.
Mke hana amri juu ya mwili wake bali mumewe vivyo hivyo mume hana
amri juu ya mwili wake bali mkewe. Msinyimane, isipokuwa mmepatana kwa
muda ili mpate faragha kwa kusali, mkajiane tena shetani asije
akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.
Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza, wala hapo si mimi, ila
Bwana (Mungu), mke asiachane na mumewe, lakini ikiwa ameachana naye na
akae asiolewe au apatane na mumewe, tena mume asimwache mkewe.
KIKAO CHA JUMAMOSI KUMALIZIA
Chanzo kilisema kuwa, kikao cha
mwisho ambacho kitamalizia kuweka mambo sawa ili wawili hao waanze ngwe
ya pili ya ndoa yao ambayo inaaminika itakuwa ya mwisho mpaka kifo
kiwatenganishe, kinatarajiwa kufanyika leo jijini Dar es Salaam mahali
ambapo hapakutajwa.
MWANASHERIA ATAJWA
Mwanasheria wa Flora aliyejulikana kwa jina
moja la Ado ametajwa kusimamia kikao hicho ili wawili hao waanze maisha
mapya baada ya safari fupi ya mvurugano uliowafanya kuwa mbalimbali.
AONGEA NA RISASI JUMAMOSI
Juzi, Risasi Jumamosi lilimsaka
mwanasheria huyo kwa njia ya simu yake ya mkononi ili kumsikia anasemaje
kuhusu kutajwa kwenye usuluhishi wa ndoa hiyo ambapo alipopatikana
alisema:
“Niko Arusha, Ijumaa nitarudi Dar. Kuhusu kikao cha
usuluhishi siwezi kukwambia lakini suala la kuwapatanisha nalifahamu,
nawaomba na ninyi msaidie kufanikisha jambo hilo zuri.”
VIPI KUHUSU KESI YA MADAI YA KUBAKA?
Hata hivyo, Wakili Ado
hakutaka kugusia kuhusu kesi ya Mbasha iliyopo Mahakama ya Wilaya ya
Ilala ambapo anadaiwa kumbaka shemejiye mara mbili (jina tunalo) ambayo
kwa mujibu wa mahakama, upelelezi umekamilika na itasikilizwa Julai 17,
mwaka huu.
KWA UPANDE WAKE FLORA
Risasi Jumamosi lilimwendea hewani, Flora ili kumsikia anasemaje kuhusu kuwepo kwa upatanishi kati yake na mumewe, Emmanuel.
Huyu hapa: “Ongea na wakili wangu atakwambia kila kitu.” Ambapo
majibu ya wakili yalikuwa: ”Ninachojua mimi ni kwamba Flora
ameshamsamehe mumewe na yuko tayari kuanza ukurasa mpya.”
MBASHA SASA
Kwa upande wake, Mbasha alipozungumza na gazeti hili juzi alisema kurejea upya kwa ndoa yake ni jambo la kuupendeza moyo wake.
“Mimi sina neno nipo tayari, nimeshasamehe yaliyotokea, Flora ni mke wangu jamani, nampenda sana kutoka moyoni.”