SIRI nzito ya mauaji ya kinyama ya mwanafunzi wa Chuo cha Savanna
Bridge cha jijini Arusha, Winfrida Akunay (18) aliyechomwa kisu mara
sita eneo la shingo na kifua mbele ya baba yake mzazi imegundulika,
Amani linakupatia.
Kwa mujibu wa chanzo cha ndani, mtuhumiwa wa mauaji hayo, Robert
Isaac (22) alitimiza ukatili huo
nyumbani kwa baba wa marehemu Majengo
Juu jijini hapa, Machi 25, mwaka huu, saa 2:12 usiku.
Ishu kubwa iliyojitokeza ni wivu wa mapenzi ambapo mgogoro mzito uliibuka kwa wawili hao.
Gazeti hili lilifuatilia kwa makini sakata la mauji hayo na
kufanikiwa kupata waraka wa siri ulioandikwa na mtuhumiwa huyo ambapo
sehemu ya waraka ilisema:
"Nakupa wiki moja ya kufikiria, kama utaendelea na msimamo wako wa
kutokuwa na mimi nitakuua kwa mikono yangu mwenyewe na mimi kujiua."
Mwenyekiti wa Mtaa wa Remtula, Majengo alisema baada ya mauaji hayo
kesho yake walikwenda nyumbani kwa mtuhumiwa eneo la Ngusero alipokuwa
akiiishi na mjomba wake na kufanya upekuzi chumbani ambapo walikuta
karatasi iliyoandikwa:
"Mimi Robert Isaac nikiwa na akili timamu, nilikuwa na marehemu
Winfrida kama wachumba kwa muda wa miaka miwili iliyopita, tuliahidiana
kuoana baada ya kula yamini ya damu, lakini ilipofika mwezi wa pili,
mwaka huu, marehemu alinikataa, lakini mwezi wa tatu tulifanikiwa
kurejesha mahusiano mara tatu.”
Unaendelea: ‘’Baadaye ndani ya mwezi huohuo, marehemu alibadilika na
kuniambia hanitaki tena, nilimpa wiki moja afikirie na kubadilisha
msimamo wake huku nikimkumbusha juu ya kiapo chetu cha damu kwamba kifo
kitutenganishe.’’
Waraka huo unaendelea: ‘’Nilimwambia kama hutabadili msimamo wako
nitakuua kwa mikono yangu miwili na kisha nami kujiua, nimemwachia
mdogo wangu shamba na baadhi ya vitu vyangu akabidhiwe yeye.”
Akizungumzia mauaji hayo, baba mzazi wa marehemu, Paul Akunay (59)
ambaye alilazwa katika Hospitali ya Kanisa Katoliki, Saint Elizabert
jijini hapa baada
ya kujeruhiwa kwa kisu mguuni na mkononi wakati akimwokoa mtoto wake, alisema:
“Siku ya tukio mtuhumiwa alifika nyumbani majira ya saa 2 usiku na
kumtaka binti yangu wazungumze walau kwa dakika moja, nilimweleza
aondoke.
“Mtuhumiwa aligoma kuondoka, badala yake alisonga mbele
hatua moja akimwelekea marehemu alipokuwa amekaa kisha akachomoa kisu
kwenye koti na kumchoma marehemu shingoni.
Nilijaribu kumshika lakini nilijikuta nikishika makali ya kisu na
kunijeruhi mkono wa kushoto na baadaye alinichoma mguuni, nikamwachia
ambapo alimrudia mwanangu na kuendelea kumchoma zaidi ya mara sita
kifuani na shingoni akirudiarudia. Alifanikiwa kukimbia.
Mzee huyo alidai hakuwahi kumwona kijana huyo hata siku moja na siku
hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza na wala hatambui uhusiano wake na
marehemu.
Marehemu Winfrida alizikwa kijijini kwao, Makuyuni wilayani Monduli, Arusha, Machi 29, mwaka huu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema polisi bado wanaendelea kumsaka mtuhumiwa huyo.




