Wiki
moja baada ya kuandikwa habari kuhusu hatari ya kupata magonjwa,
ikiwemo kipindupindu inayowakabili wakazi wanaoishi karibu na dampo la
Pugu Kinyamwezi na hatua ya kula kwenye chandarua walioianzisha
kupunguza kero ya inzi, uongozi wa Jiji la Dar es Salaam umezungumzia
hali hiyo.
Mkurugenzi
wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe amekiri kuwepo kwa tatizo la
hatari ya magonjwa kwa wakazi hao, lakini amesema wakazi hao ni wavamizi
wa eneo la kutupa takataka kwa kuwa walilikuta dampo wakati wakijenga
eneo hilo hivyo wanapaswa kuondoka.
Alisema
kutokana na kuvamia eneo hilo, adha wanazopata, wamejitakia wenyewe na
kuwaeleza kuwa dawa ya kumaliza adha hizo ni kuondoka kama
walivyoelekezwa na Serikali mara nyingi kupitia viongozi mbalimbali
akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk Mohammed Gharib Bilal.
"Wale
ni wavamizi wa eneo la kutupa taka, dawa ya mvamizi si kulalamika
kwamba yupo hatarini kupata magonjwa, ni kuchukua hatua kukabiliana na
tatizo hilo ikiwemo kuondoka eneo hilo, serikali ilishawataka mara
nyingi waondoke lakini ndio tabia zetu wananchi, hawataki kuchukua hatua
hiyo," alisema Kabwe alipozungumza na gazeti hili Ijumaa.
Alipoulizwa
muda waliopewa wakazi hao kuondoka, Kabwe alisema serikali kwa kutambua
kuwa wale ni wanadamu kama wengine, wamepewa muda mrefu wa kuondoka
taratibu na kutaka wengine wasiendelee kujenga eneo hilo lakini bado
hakuna waliochukua hatua hiyo.
Kabwe
alisema masuala ya siasa pia yanaingilia suala hilo, jambo linaloweka
ugumu kuchukua hatua na kuongeza kuwa yanayoendelea Pugu ni kama
yaliyotokea Jangwani ambako pamoja na wakazi hao kukumbwa na mafuriko na
hata wengine kupoteza maisha, waling'ang'ania kuishi eneo hilo pamoja
na kutengewa eneo la Mabwepande, Kinondoni jijini humo.
Hata
hivyo, Kabwe alipoulizwa kwanini wakazi hao wa dampo la Pugu Kinyamwezi
lililopo wilayani Ilala wasitengewe na wao eneo, alisema wakazi wa
Jangwani kupewa Mabwepande ilikuwa ni huruma ya Serikali na kueleza
kwamba, si kila wakati Serikali itafanya huruma kama huo.
Kuhusu
hali ya inzi na miundombinu mibovu ya dampo hilo, Kabwe alisema kwa
wiki mbili sasa wamekuwa wakipiga dawa na hata siku alipozungumza na
mwandishi, Ijumaa iliyopita, walipiga dawa.
Akizungumzia
mpango wa kulifanya dampo hilo kuwa la kisasa, Kabwe alikiri kweli kuwa
miundombinu ya dampo hilo haiko vizuri na kueleza kuwa, mpango wa
Serikali ni kuliboresha unaendelea. Hata hivyo hakutaka kueleza hatua
ilikofikia zaidi ya kudai mchakato uanendelea.
Miongoni
mwa malalamiko ya wakazi hao ni ahadi ya serikali kuwa dampo hilo
lingekuwa la kisasa, likizungushiwa ukuta, kuwekewa dawa ya kuzuia
madhara kwa binadamu. Tofauti na hayo, dampo hilo liko wazi, lililojaa
nzi na wadudu wengine wa hatari, na mvua zinaponyesha, maji machafu
hutiririka kwenye makazi ya watu.
Hivi
karibuni mwandishi alifika katika dampo hilo na kubaini kuwa, wakazi
waishio karibu na eneo hilo katika harakati za kujikinga na maradhi na
usumbufu wanaoupata wa nzi majumbani, wamegundua mbinu mpya za
kukabiliana na tatizo hilo na sasa familia zinakula chakula ndani ya
vyandarua.
Familia
hizo hulazimika kufunga chandarua ama sebuleni au barazani na baba,
mama, watoto na wanafamilia wengine huingia ndani yake na kuzuia vizuri
mianya ya nzi kuingia kwa kuweka mawe ama mbao na kisha hupata ahueni ya
kula bila kuandamwa na nzi.
Hata
hivyo, pamoja na ugunduzi huo uliotoa nafuu kwa kuwapunguzia maradhi,
hali za afya kwao bado ni tete kutokana na harufu kali ya kemikali na
taka zinazotupwa katika dampo hilo pamoja na hatari ya kupata saratani
kutokana na moshi unaofuka mara kwa mara.
Baadhi
ya wakazi wa eneo hilo waliozungumza na gazeti hili katika makazi yao
umbali wa kutengwa na barabara inayoingiza magari yanayotupa taka eneo
hilo, walilalamikia hali hiyo na kueleza kuwa wameamua kugundua mbinu
hiyo ili kunusuru afya zao.
Maua
Hamis (22), mkazi wa Mtaa wa Kichangani Majohe, alisema watoto katika
familia wamekuwa wakiugua vifua, matumbo ya kuhara, mafua na malaria
kila kukicha kutokana na madhara ya dampo hilo na familia takribani
zote, sasa wanalazimika kununua vyandarua zaidi ya viwili kwa ajili ya
matumizi hayo.
"Hapa
kwetu 'neti' (chandarua) hazina kazi ya kuzuia mbu tu usiku au mchana,
bali tunazo zaidi ya mbili na familia nyingi tunazitumia kwa chakula
pia, tunazifunga kwa kamba ama misumari ukutani sebuleni ama barazani na
tunaweka mawe, vipande vya miti au mbao kwa chini ili nzi wasiingie
kisha tunaingia wote haraka haraka na kuanza kula tukiwa ndani ya neti,"
alisema Maua.
Alisema
mara zote wanapotaka kula iwe chai, mlo wa mchana ama usiku
wanalazimika kufanya hivyo kwa kuwa jambo la ajabu ni kwamba nzi hao
hawalali hata usiku ni wasumbuu kama wanavyofanya mchana.
Mwandishi
akiwa eneo la tukio, alishuhudia wingi wa nzi hao katika bustani za
mboga katika makazi ya watu, kwenye magudulia ya maji, ukutani na
walikuwa wakitua na kuruka kwa wingi kwa watu, akiwemo mwandishi wa
habari hizi. Awali waandishi walipofika eneo hilo na kuvuta hewa,
walianza kuumwa matumbo na vichwa.
Watoto
walionekana pembezoni mwa dampo wakicheza huku nzi wakiwa midomoni,
puani na maeneo mengine ya mwili, maji machafu kutoka katika dampo
yakiwa yanapita na kuingia katika makazi yao huku watoto hao wakicheza
kwenye maji hayo bila viatu. Baadhi ya watu walionekana katikati ya
dampo wakiokota vyuma chakavu, chupa na vifaa vingine bila vifaa vya
kinga.
Moses
Lucas, mkazi wa eneo hilo alidai hali za afya kwa wakazi wa eneo hilo
ni tete kutokana na mazingira yaliyopo hasa nyakati hizi za mvua na
kuongeza kuwa, japo wanakula kwenye chandarua lakini watoto wanacheza
kwenye maji machafu kutoka katika dampo hilo.
Lucas
alisema kumeundwa kamati ya wananchi kushughulikia kero hizo, lakini
alidai serikali imekuwa ikiwapiga danadana katika kushughulikia kero
hizo ikiwemo kuboresha dampo.
Baadhi
ya watoto waliozungumza na mwandishi, Rashid Abdallah (12) na Bariki
Massawe (11) walisema kwa nyakati tofauti kuwa wanalazimika kufukuza nzi
ndani kwa muda wa nusu saa kabla ya kuweka neti na kula chakula, pia
moshi, harufu na maji machafu yanahatarisha afya zao.
