SHABIKI
yeyote atakayeingia uwanjani na mnyama yeyote iwe kuku au njiwa
atakumbana na rungu la sheria ya kufungwa jela siku 90 au faini ya Sh.
100,000.
Katika siku za hivi karibuni baadhi ya mashabiki wamekuwa na kawaida
ya kuingia uwanjani na ndege wakiwemo kuku au njiwa na kuwashikilia muda
wote wa mchezo kitendo kinachozua usumbufu kwa mnyama.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mkurugenzi wa Taasisi ya Ustawi wa Wanyama
Tanzania (Taweso), Dk. Thomas Kahema alisema, mtu yeyote anayeingia na
wanyama uwanjani anapaswa kuhakikisha anampatia huduma muhimu mnyama
vinginevyo anashtakiwa kwa mujibu wa sheria ya wanyama ya mwaka 2008.
“Sheria ipo wazi, tukimkuta mtu wa aina hiyo anapigwa faini ya Sh.
100,000 au anaenda jela kwa muda wa miezi mitatu, hairuhusiwi kubughudhi
wanyama, pale uwanjani kuna kelele na huwa wanawanyima uhuru wanyama,”
alisema Kahema.
Naye Mkuu wa Vikosi vya Mbwa na Farasi wa Jeshi la Polisi Tanzania,
Mrakibu Mwandamizi Dk. Eugene Emmanuel aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Huo
ni ukatili wa wanyama na hairuhusiwi kuingia na mnyama yeyote uwanjani
bila sababu ya msingi, nazungumza na askari wangu kuwapa agizo kumkamata
yeyote atakayeingia na ndege uwanjani bila sababu ya msingi.”
Hata hivyo shabiki wa Yanga, Ally Ramadhani, ambaye amekuwa
akionekana na kuku mara nyingi Uwanja wa Taifa amewahi kuliambia gazeti
hili kwamba huwa anaingia na kuku huyo uwanjani kwa imani ya timu yake
kupata mabao.
Aliingia na kuku mmoja Yanga ilipocheza na Al Ahly katika Ligi ya Mabingwa Afrika na timu hiyo ikashinda bao 1-0.
SOURCE: MWANASPOTI
SOURCE: MWANASPOTI