NIMEWAHI
kukaa zaidi ya miezi sita bila kufika mjini. Wenye jiji lao wanakuambia
Dar es Salaam mjini ni maeneo ya Posta, kule kwenye mitaa ya Ohio,
Indira Ghandi, Samora, Sokoine, Zanaki, Azikiwe, Magogoni, Garden,
Maktaba na kadhalika.Eti ukisema unaenda au ulikuwa mjini, basi mjanja anajua ndiyo kule, lakini vinginevyo sema nipo au nakwenda Mwenge, Magomeni, Kariakoo, Ilala, Temeke, Ubungo, Kigogo, Kigamboni, Kinondoni, Kawe, Tegeta, Boko, Kimara, Buguruni, Ukonga, Gongo la Mboto, Vingunguti, Tandika, Keko, Kurasini na maeneo mengine yote ya nje ya mji.
Na kama unavyojua msemo wa siku hizi, ‘Uzee Mwisho Chalinze, Mjini Kila Mtu Baby.’ Basi siku moja nilikuwa mjini, sehemu moja hivi inaitwa Steers. Wanauzaga vinywaji baridi. Meza niliyochagua kukaa, alikaa mtoto mmoja wa kike, kwa kumtazama, asingeweza kuwa na umri wa kuzidi miaka 18.
“Habari yako,” nilimsalimia kwa heshima ya umri wangu, nikitaraji kabisa ‘kupigwa’ na shikamoo. Lakini unajua binti alinijibuje?
“Poa, mambo?”
Kwa kuwa mjini kila mtu Baby, sikutaka kung’ang’ania uzee, ambao nilishauacha Tegeta, ikabidi mara moja nirejee ujana na maisha yakaendelea.
Nilikuwa mtu mzima, nikaamua kuutumia umri wangu kwenda na hali halisi, lakini binti akanigeuza, akaona naleta uzee katika sehemu za vijana. Kwangu ilikuwa poa tu, maana haya ndiyo maisha tunayoishi huku uswahilini, mtoto ni wako, wa mwenzio mkubwa mwenzako!
Sikia kisa hiki kingine. Jamaa mmoja mtu mzima, anayekaribia miaka 50, alienda katika hoteli moja iliyopo ufukweni mwa Bahari ya Hindi. Akamuona binti mmoja amevaa ‘ki-beach beach’, amejilaza mchangani, akamsogelea na kumwambia “Mambo mtoto mzuri? Uko bomba sana.”
Binti akamtazama jamaa, kisha kwa dharau akamwambia “Lione kwanza, baba mtu mzima huna hata haya, mimi si kama mwanao tu!”
Mzee mzima likamshuka. Lakini kama ilivyonitokea tu, kwa kuwa mjini hakuna mzee, haraka akamkabili yule binti.
“Acha ushamba wewe, baba yako anaweza kukupa bata? Anaweza kukununulia Blackberry, kukupeleka kula raha Zanzibar asubuhi na kurudi jioni, au hao vijana wenzako watakupa nini zaidi ya kukunukisha shombo? Twende kwenye gari tuhame hapa nikupe maisha wewe..!!”
Binti akamtazama mtu mzima, akagundua alifanana na maneno yake, taratibu tabasamu likachanua, uzee ukaachwa Chalinze, wakaanza kuitana Baby, Baby!
Haya ndiyo maisha wanayokutana nayo watu wazima na watoto wa shule. Kuna vishawishi kila upande, madenti wana nafasi yao na watu wazima wana nafasi yao, nani wa kulaumiwa tunapozungumzia upotevu wa maadili?
Akina mama walioolewa na hata wale wenye wapenzi tu, wanawalalamikia wanafunzi kuwa ni hatari kwa ndoa na uhusiano wao. Mabinti wakipewa lifti kwenye magari, wanatumia muda mwingi kuonyesha sura ya ‘poa tu’ na watu wazima wengi ni dhaifu, hasa wanapokutana na mabinti ambao bado ‘wananuka maziwa ya mama zao’ kama wenyewe wanavyosema!
Hii ni mada pana, ambayo ni vigumu kidogo kuijibu kirahisi kwa sababu ina vyanzo vingi. Ningependa sana kushirikiana na wadau wote, wakiwemo wazazi, wanafunzi wenyewe na hata wale ambao walisoma muda mrefu uliopita na sasa wapo mtaani wakiendelea na harakati za maisha.
Lengo hapa ni kujaribu kuangalia uwezekano wa kumaliza tatizo la watu wazima kushiriki mapenzi na watoto wa shule. Tatizo haliwezi kumalizika mara moja bila kujua chanzo, dalili na mbinu zinazotumiwa na makundi yote.
Tatizo lipo kwa madenti au watu wazima? Unaweza kushiriki kutoa kisa unachokijua, kilichokutokea ukiwa kama mzazi, denti au shuhuda, toa maoni yako kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno kupitia namba zangu za simu au kunipigia kama utakuwa na salio.