Ni Daktari alieonyesha moyo wa kuendelea na kazi licha ya kupata maradhi ya kiharusi yaliyomsababishia kupooza mkono na mguu. Hapana
shaka kuwa maelfu ya wanawake nchini waliowahi kupata huduma zake
wanamkumbuka bado kwa msaada mkubwa aliowapa na kuwasaidia kushika
mimba, kuwapa ushauri wa kitaalamu au hata kuwazalisha. Licha ya kustaafu, atabakia kukumbukwa kwa mengi hapa nchini, hasa kwa mchango wake kwenye sekta ya afya ya mama na mtoto.
Huyu si mwingine, bali ni
Profesa Malise Kaisi (pichani), Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake
na Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi ya Tiba
(Muhas). Nafika nyumbani kwake maeneo ya Mikocheni jijini Dar es Salaam na ninamkuta akiwa amejipumzisha. Anaanza kwa kunipa historia yake fupi ya kikazi.
Atoa damu kuokoa wagonjwa - Nia ya daktari yeyote duniani, ni kuokoa maisha ya mgonjwa. Hiyo ndiyo faraja ya wataalamu wa afya walio wengi.
Akiwa ni
daktari ambaye anaipenda kazi yake, Profesa Kaisi amewahi kujitolea damu
kuwaokoa wagonjwa wake katika dakika ambazo pengine walikuwa kwenye bonde la uvuli wa mauti.
“Unajua
wakati ule, damu ilikuwa ni tatizo kubwa. Hakukuwa na benki ya damu kama
ilivyo sasa, hivyo unapopata mgonjwa anayehitaji damu na yupo mikononi
mwako, lazima ujitoe mhanga” anasema
Anakumbuka
mwaka 1970 ambapo alimpokea mgonjwa aliyepata ajali mbaya na alihitaji
damu. Ilibidi ajitolee damu yake ili kumwokoa mgonjwa yule.
“Nikiwa
Newala mwaka 1970 huo huo, mgonjwa wangu aliyekuwa anajifungua aliishiwa
damu sana na ikabidi nitoe damu yangu haraka sana na kumuwekea na
alipona,” anasema
Mara nyingine
akiwa ndiyo kwanza ameripoti kwenye kituo kipya cha kazi huko Mtwara,
alifika na kumkuta mgonjwa akiwa kwenye hali mbaya na hakuwa na mtu wa
kumpa damu hivyo alikuwa akisubiriwa kufa, yeye alitoa damu yake na
mgonjwa akapona.
“Cha muhimu
ni kufahamu kama una maambukizi au la. Ukishajijua, unatakiwa utoe damu
kama wewe ni daktari,” anasisitiza Profesa Kaisi.
Azalisha kwa kutumia IVF - Profesa Kaisi, ni daktari wa kwanza Mtanzania kuzalisha kwa njia ya IVF hapa nchini na kufanikiwa kusababisha mimba zaidi ya 11 kutungwa kwa njia hiyo.
IVF ni mchakato wa utungishwaji wa mimba kwa upandikizaji wa mbegu za mwanamke na mwanaume kwenye nyumba ya uzazi ya mwanamke.
Anasema akiwa na daktari kutoka Korea , Otman Bauer, walifungua Kliniki ya majaribio mwaka 1989 ambayo ilikuwa ikiwasaidia wanawake walioshindwa kushika ujauzito.
Wanawake
waliozalishwa kwa njia ya IVF ni wale ambao walikuwa hawawezi kushika
ujauzito kwa sababu kama vile mirija ya kupitisha mayai kukatika, mayai
kushindwa kupevushwa au kuwa na maradhi mengine yanayozuia utungishwaji
wa mimba.
IVF hufanyikaje? - Profesa
Kaisi anasema, yai la mama hupevushwa kwa kutumia dawa maalumu na
hufuatiliwa kwa kutumia mashine ya uchunguzi wa ndani ya mwili (ultrasound).
“Baada ya
yai kukomaa, sindano maalum yenye wembamba mithili ya unywele huingizwa
ukeni hadi kwenye mirija na yai lililopevuka huchukuliwa na kutolewa
nje” anasema
Yai au mayai hayo huwekwa kwenye chombo maalumu (test tube) kabla ya kuhamishwa kwenye beseni maalumu ambalo litalifanya liendelee kuwa hai licha ya kutoka nje ya mwili wa binadamu.
“Beseni hilo
halina budi kuwa na mazingira kama ya mwilini, kwa mfano joto, mwanga
na kusiwepo na sauti, kwani yai huweza kuharibika kwa kasoro ndogo ndogo
sana,” anasema
Anaongeza
kuwa wakati huo mbegu za mwanaume hupimwa kama hazina walakini na
hutolewa kwa mwanaume kujichua au kama hawezi kujichua basi hutakiwa
kufanya tendo la ndoa na mke wake na kisha mbegu kukingwa na kuwekwa
kwenye chombo maalumu.
Mbegu za baba, hutakiwa kutolewa saa mbili mara baada
ya yai la mama kutolewa ili visipishane. “Baada ya yai na mbegu
kutolewa, hatua inayofuata ni kuichoma mbegu kwenye yai kwa kutumia
sindano maalum. Mchakato huu unaitwa kwa kitaalamu, Intra Cytoplasmic
Sperm Injection au ICSI), ” anasema.
Anaeleza
kuwa, baada ya mbegu na yai kuchanganywa, huwekwa kwenye chombo maalum
cha joto kitaalamu ‘Incubator” kwa saa 40 kabla ya kuwekwa au
kupandikizwa kwenye kizazi cha mama.
“Hali kadhalika, ‘incubator’ inatakiwa kuiga hali ya tumboni mwa mama wakati yai la mama na mbegu za baba vinapowekwa kabla ya kuwekwa kwenye kizazi cha mama, kwa mfano joto, mwanga na sauti” anasema Profesa Kaisi.
Hata hivyo,
Profesa Kaisi anasema IVF ina mafanikio makubwa kwa mtu yeyote
isipokuwa wanawake wenye umri wa miaka 40 na kuendelea .
Anaeleza zaidi kuwa, wanawake walio wengi hudhani kuwa ni wagumba, lakini kumbe hawajafahamu matatizo yao.
Umuhimu wa madaktari - Profesa Kaisi anasema, bado madaktari nchini hawapewi umuhimu unaolingana na kazi yao, bado hawathaminiwi kwa mchango wao.
Kwa mfano,
anasema, hakuna mtu anayejali kuwa madaktari hufanya kazi kwa saa 24 na
wakati mwingine kukosa wakati wa kupumzika hata na familia zao.
“Wakati mwingine mimi nilikuwa nakosa hata muda wa kuonana na watoto wangu. Zinapita hata siku tano, sijawaona watoto” anasema
Anasema, viongozi wengi hawafahamu umuhimu wa madaktari ndiyo maana wanakwenda kutibiwa nje.
Historia yake - “Kabla
ya kuingia chuo kikuu, nilibahatika kusoma Shule ya Sekondari ya
Wavulana Tabora, ambako nilisoma na Samwel Sitta (Waziri wa Ushirikiano
wa Afrika Mashariki), Joseph Mungai na Muhidin Ndolanga, ” anasema
Anasema
alianza kazi Hospitali ya Muhimbili (sasa Hospitali ya Taifa), mwezi
Aprili mwaka 1969 baada ya kumaliza Shahada ya Udaktari.
Profesa Kaisi, alishika nafasi hiyo hapo Muhimbili kwa muda mfupi kabla ya kuhamishwa Hospitali ya Mawenzi iliyoko Moshi Mkoani Kilimanjaro mwaka 1970. Mwaka 1971 alichaguliwa kuwa Daktari Mkuu wa Mkoa wa Mtwara (RMO).
Anasema
alipata nafasi ya kujiendeleza kielimu ambapo mwaka 1973 alikwenda Chuo
Kikuu Kishiriki cha Tiba cha Muhimbili (Muhas) ambako alibobea kwenye
masuala ya tiba ya magonjwa ya wanawake hasa ugumba.
Kwa elimu hiyo, alikuwa ni daktari bingwa wa kwanza nchini wa magonjwa ya wanawake.
Aliendelea
na kazi hadi mwaka 1976 ambapo alitakiwa kuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu
Kishiriki cha Tiba (Muhas) kazi aliyoifanya hadi mkwaka 1998
alipostaafu.
Hata hivyo, kutokana na unyeti wa taaluma yake, Profesa Kaisi hakustaafu moja kwa mojabali alipata mkataba wa kuendelea kufundisha hadi serikali ilipotengua mikataba yao Novemba mwaka jana.
Profesa Kaisi anasema, kutokana na kubobea kwenye masuala ya uzazi kwa wanawake, aliamua kuanzisha huduma ya mama na mtoto ili kuwasaidia wanawake vijijini.
“Niliomba
fedha kwa wafadhili kwa ajili ya mafunzo kwa wakunga ambao walikwenda
mkoani Mtwara kuwasaidia wanawake walioathiriwa baada ya vita iliyokuwa
ikiendelea Msumbiji wakati huo” anasema
Anasema huduma hiyo ilisaidia sana wanawake wengi kupata huduma ambayo ilipunguza vifo vya mama na mtoto maeneo ya vijijini.
Anamaliza
kwa kusema: “Madaktari si mashetani wala malaika, wanapogoma
wasilaaniwe, bali maslahi yao yaangaliwe upya kwani kazi yao ni ngumu.”
Chanzo - Mwananchi