
Mwanafunzi akifungasha virago tayari kuondoka shuleni
Mwanafunzi
mmoja nchini Kenya ameuawa kwa kupigwa na watu wanaoshukiwa kuwa
majambazi ambao walivamia shule moja viungani mwa mji mkuu Nairobi.
Mwanafunzi
huyo na wenziwe walikuwa wamelala kwenye bweni lao katika Shule ya St.
Charles Mutego iliyoko katika kitongoji cha Dagoreti, Magharibi mwa
Nairobi.
Inaarifiwa
watu hao walivamia shule hiyo na kuzima taa na baadaye kuvunja
madirisha ya vioo pamoja na magari yaliyokuwa yameegeshwa shuleni hapo
na kisha kuwapiga wanafunzi waliokuwa wamelala.Wanafunzi wengine 50
walijeruhiwa.
Mkurugenzi
mkuu wa shule hiyo Charles Niyamote ameiambia BBC kuwa kiini cha
mashambulizi haya huenda ikawa ni wivu, kwa sababu wanaona shule hiyo
ina watoto wengi. Walipokuwa wakitekeleza uhalifu huo, waliwaambia
watoto hao waitoroke shule hii.''
Polisi
walidhibitisha tukio hilo lakini walikataa kutoa taarifa hadi
watakapokamilisha uchunguzi wao. Hakuna mshukiwa aliyekamatwa hadi
kufikia sasa.
Kwa sasa shule hiyo imefungwa kwa muda wa wiki moja wakati polisi wakiendelea na uchunguzi wa kina.
Visa vya
ukosefu wa usalama vimeongezeka katika mji wa Nairobi na maeneo mengine
ya Kenya katika siku za hivi karibuni, lakini si jambo la kawaida kwa
wanafunzi kuvamiwa kwa njia hii wakiwa shuleni.