Masanja Mkandamizaji si jina geni
masikioni mwa watu wengi kutokana na uwezo wake wa kuwavunja mbavu
watazamaji pale anapoonekana katika runinga na Kundi la Original Comedy.
Licha ya kufika hapo alipo sasa, anakiri
wazi kuwa amepitia katika maisha magumu hususani wakati alipoamua
kuanza maisha binafsi ya kujitegemea baada ya kutoka nyumbani kwa dada
yake alipokuwa akiishi.
Anasema kabla ya kuondoka kwa dada yake
alimuomba amtafutie chumba ili ajitegemea na kuanza maisha binafsi kama
kijana . Nilimwambia dada anitafutie chumba na alifanya hivyo ingawa
alikuwa anahofia kama nitaweza ,basi nikapata 'geto' langu maeneo ya
Tabata Aroma na nilitakiwa kulipa kodi ya TSh. 5,000 kwa mwezi, anasema
Masanja. Anakiri wazi kuwa changamoto katika maisha ndizo zilizochangia
kumfikisha mahali alipo sasa kwani licha ya kuwa katika hali ngumu
Hakukata tamaa bali alizidi kujituma kwa
nguvu zake zote. Anasema kuna wakati ilikuwa vigumu kuipata hata hiyo
hela ya kodi kwahiyo ilikuwa inamlazimu kurudi kwa dada yake kwa muda
unapofikia wakati kulipa kodi. Yaani hiyo TSh. 5,000 kuipata ilikuwa
shughuli maana ilikuwa ikifika karibu na mwisho wa mwezi narudi kwa dada
kuzuga kidogo ili mama mwenye nyumba ajue nimesafiri,anasema. Anasema
alianza kwa kulala chini mpaka siku alipofanikiwa kupata fedha kidogo
iliyomuwezesha kununua godoro la sufi jambo ambalo anajivunia nalo kwani
aliweza kununua kwa jasho lake.
Anaongeza kuwa kamwe hawezi kumsahau
marehemu Steven Kanumba pamoja na mtu mwingine aliyemtaja aitwaye Mtitu
kutokana na mchango wao uliosaidizi kumfikisha hapo alipo sasa.
“Namshukuru sana marehemu Kanumba
alikuwa anakuja kunichukua kule Tabata tunaenda kupiga 'inshu' ambazo
zilikuwa zikiniingizia pesa kidogo iliyoniwezesha kuishi hata hivyo
maisha yalikuwa magumu. Wakati naanza maisha sikuwahi kutoa hela hata ya
kununua chipsi kavu lakini siku moja nilifanya kazi na Mtitu ambayo
alinilipa laki moja sikuamini macho yangu, kwa mara ya kwanza kununua
chipsi kuku kwani nilikuwa nikitamani mlo huo nililazimika kusaidia
kumenya viazi kwa washikaji” alieleza Masanja.
Sambamba na uchekeshaji Masanja pia
amejiingiza katika shughuli za kumtukuza Mungu baaada ya kuokoa na sasa
anafanya vizuri pia katika uimbaji wa nyimbo za injili na kesho Jumapili
atazindua albamu yake ya pili ya muziki wa Injili inayoitwa Hakuna
jipya chini ya jua.
-Habari kwa hisani ya mwandishi John Minja-
