Na Somoe Ng'itu, Dar es Salaam
WAKATI
beki wa zamani wa klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Shomary
Kapombe, anadaiwa kukataa kurejea katika timu yake ya AS Cannes ya
Ufaransa, habari zaidi zimeelezwa kwamba wakala wake amewaambia Azam
kuwa mchezaji huyo thamani yake ni Dola za Marekani 150,000.
Habari
kutoka kwa watu wa karibu wa mchezaji huyo zinasema kwamba nyota huyo
amemueleza wakala wake, Denis Kadito, atakuwa tayari kurejea Ufaransa
kucheza katika timu nyingine na si hiyo ya awali ambayo ilimpokea
akitokea Simba.
Chanzo
cha gazeti hili kinaeleza kwamba tayari mazungumzo kati ya Kapombe na
Azam yamefikia katika hatua za mwisho na ni moja ya sababu iliyomfanya
beki huyo wa timu ya soka ya Taifa (Taifa Stars) kukataa kurejea
Ufaransa.
"Tayari
Kapombe ameshamueleza wakala wake (Denis Kadito) kwamba hana nia ya
kurejea AS Cannes, na hata kama akirejea Ufaransa iwe ni kwenye klabu
nyingine," kilisema chanzo chetu.
Hata
hivyo, Kapombe, alikataa kuzungumza chochote kuhusiana na taarifa za
yeye kukataa kurejea Ufaransa na kuelezea maamuzi yake ya kuendelea
kukaa hapa nchini.
"Kwa
sasa siwezi kusema chochote, mtafute wakala wangu ndio atakayekueleza,
nisamehe sana," alisisitiza beki huyo ambaye Simba ilimsajili akitokea
Polisi Morogoro iliyowahi kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Kwa
sasa beki huyo anafanya mazoezi binafsi katika viwanja tofauti hapa
jijini Dar es Salaam ili kulinda kiwango chake kisishuke.
Afisa
Habari wa Azam, Jaffer Idd, alisema kwamba ni mapema mno kuzungumzia
usajili wa wachezaji katika muda huu ambao bado timu yao iko katika
harakati za kuwania ubingwa wa Bara.
Idd
alisema kuwa muda muafaka utakapofika na dirisha la usajili
litakapofunguliwa rasmi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ndio
wataanza zoezi hilo.
Azam
iliyokuwa inashiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho imeondolewa na
Ferroviario de Beira baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 juzi huko
ugenini.
Kadito
hakupatikana jana katika simu yake ya mkononi kueleza mikakati ya
kumrejesha Kapombe Ufaransa kama ilivyotarajiwa baada ya kumaliza
tofauti za mchezaji huyo na AS Cannes.
(Habari hii imeandikwa na Mwandishi Somoe Ng’itu wa gazeti la NIPASHE)
![]() |
| Anarudi Ufaransa; Shomary Kapombe amekubali kurejea Ufaransa, lakini akachezee timu nyingine si AS Cannes |
