BAADA
ya kufungwa mara mbili mfululizo bao moja kila mechi (Simba SC 1-1
Mtibwa Sugar na Simba SC 0-1 Mgambo JKT), kipa Ivo Mapunda alianzishiwa
benchi katika mchezo dhidi ya Mbeya City mjini Mbeya Jumamosi.
Katika
mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliofanyika Uwanja wa
Sokoine, kipa Mghana Yaw Berko alianza na akafungwa bao la penalti
kipindi cha kwanza katika sare ya 1-1.
Berko alidaka vizuri na kuwazuia Mbeya City kupata bao zaidi hadi dakika 90 za mchezo huo zinatimu.
Ivo
alifungwa mabao rahisi mara mbili mjini Morogoro katika sare ya 1-1 na
Mtibwa na Tanga Wekundu wakilala 1-0 mbele ya Mgambo, lakini hiyo
haiondoi ukweli huyo ndiye kipa bora kabisa kwa sasa nchini.
Lakini
hata Berko, aliyewahi kudakia Yanga SC kama Ivo, naye ni kipa mzuri-
hiyo inamaanisha kocha Zdravko Logarusic atalazimika kuwapanga kwa awamu
makipa hao katika mechi zijazo.
Hapendwi
mtu, hapa kazi tu: Kocha Logarusic hakutaka hata kumtazama Ivo Mapunda
wakati anaelekea kwenye benchi Jumamosi muda mfupi kabla ya kuanza kwa
mechi dhidi ya Mbeya City
Maisha mapya? Ivo Mapunda akiwa benchi na wachezaji wenzake wa akiba Jumamosi, je itamchukua muda gani hapo kurejea langoni?Atadumu langoni? Yaw Berko alidaka vizuri Jumamosi Mbeya akafungwa kwa penalti, je ataendelea kupangwa mechi zijazo?
REKODI YA IVO MAPUNDA SIMBA SC
Simba 3-1 Yanga (Nani Mtani Jembe, alifungwa moja Dar)
Simba SC 1-0 AFC Leopard (Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 0-0 KCC (Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 2-0 Chuoni (Robo Fainali Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 2-0 URA (Nusu Fainali Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 0-1 KCC (Fainali Kombe la Mapinduzi, alifungwa moja)
Simba SC 1-0 Rhino Rangers (Ligi Kuu Bara)
Simba SC 4-0 JKT Oljoro (Ligi Kuu Bara)
Simba SC 1-1 Mtibwa Sugar (Ligi Kuu Bara, alifungwa moja)
Simba SC 0-1 Mgambo JKT (Ligi Kuu Bara, alifungwa moja)
REKODI YA YAW BERKO SIMBA SC
Simba SC 3-1 KMKM (Kirafiki, alifungwa moja Dar)
Simba SC 1-0 KMKM (Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 0-1 Mtibwa Sugar (Kirafiki, alifungwa moja)
Simba SC 1-1 Mbeya City (Ligi Kuu Bara, alifungwa moja)
Awali
ilionekana kama Ivo ambaye alifanya kazi na kocha huyo Mcroatia Gor
Mahia ya Kenya angekuwa ‘panga pangua’ hakosekani kikosini, lakini mechi
mbili za ugenini za Ligi Kuu zimebadilisha upepo.
Kwa
kuwa Berko alidaka vizuri Mbeya, wazi ana nafasi kubwa ya kuanzishwa
katika mchezo ujao pia wa Ligi Kuu na kama ataendelea kufanya vizuri,
ina maana itabidi Ivo asubiri hadi Mghana huyo aboronge ndipo arejeshwe
langoni.
Yote
kwa yote, ni jambo zuri kwa timu kuwa na makipa bora wa aina ya Ivo na
Berko kikosini, kwani ushindani wao wa nafasi ya kuanza, unafanya lango
la Simba SC liwe kwenye mikono salama.
Hadi
sasa, Ivo Mapunda ameidakia Simba SC mechi 10 tangu Desemba 21, mwaka
jana akifungwa mabao manne tu, mbali na mawili ya Ligi Kuu, lingine
alifungwa katika Fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya KCC na lingine
katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Yanga mechi ya Nani Mtani Jembe.
Berko
katika mechi nne alizoidakia Simba SC tangu Desemba mwaka jana,
amefungwa mabao matatu na mechi pekee ambayo alimaliza dakika 90 bila
kuokota mpira nyavuni ilikuwa dhidi ya KMKM ya Zanzibar Kombe la
Mapinduzi hatua ya makundi.
Je,
Ivo baada ya kusugua benchi Jumamosi, itamchukua muda gani kurejeshwa
langoni Simba SC? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.





