BIN ZUBEIRY imefanikiwa kupata nakala ya barua hiyo iliyotumwa nchini Februari 12, mwaka huu kutoka makao makuu ya shirikisho hilo, Zurich kwenda kwa Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa Dar es Salaam na FIFA imesema yenyewe haihusiki na usajili wa mchezaji, bali ni shirikisho la nchi husika.
Okwi akiichezea Etoile msimu huu |
Okwi akiichezea SC Villa Oktoba 22 mwaka jana katika ligi ya Uganda na akafunga bao katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Bright Stars |
Okwi akishangilia bao lake SC Villa |
Barua ya FIFA imeiagiza TFF ifuate kanuni na taratibu za usajili katika suala la mchezaji huyo.
FIFA pia imesema inatambua Okwi alihamishwa kutoka Simba SC Januari 15, mwaka jana kwenda Etoile du Sahel ya Tunisia kwa Mkataba wa kudumu na baadaye, kufuatia uamuzi wa jaji mmoja baada ya mchezaji huyo kufungua kesi FIFA, aliruhusiwa kuchezea SC Villa ya Uganda kwa muda Oktoba 5, mwaka jana.
FIFA pia imesema inatambua Okwi alihamishwa kutoka SC Villa kujiunga na Yanga SC Desemba 15, mwaka jana, lakini imesistiza TFF ifuate taratibu na kanuni za usajili, tena ikiielekeza vipengele vya kupitia katika kumaliza kesi hiyo.
FIFA pia imesema inatambua Simba SC inadai fedha za kumuuza Okwi Etoile, lakini imesema hiyo ni kesi tofauti na suala la uhalali wa mchezaji huyo Yanga SC.
Ikumbukwe, TFF iliiandikia FIFA kutaka ufafanuzi wa mchezaji huyo kama wanaweza kumhalalisha kuchezea Yanga na baada ya kupokea, majibu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Mwesigwa alizungumza na BIN ZUBEIRY akasema suala hilo limekwisha na mchezaji huyo yuko huru kuchezea Yanga.
Kama maelezo ya Mwesigwa yalikuja baada ya kufuata maelekezo ya FIFA, yaani kupitia kanuni na taratibu za usajili wakajiridhisha Okwi anaweza kuwa sahihi kuchezea Yanga, basi klabu hiyo haitakuwa matatani ikimtumia mchezaji huyo.
Lakini kama tu baada ya kupokea barua hii, TFF ikaamua kumruhusu Okwi kuchezea Yanga SC bila kufuata maelekezo ya FIFA, iwapo kanuni na taratibu za usajili zikimbana mchezaji huyo basi klabu hiyo inaweza kuwa matatani baadaye.
Wazi Yanga inaweza kupokonywa ushindi katika mechi zote ambazo itamtumia Okwi, iwapo baadaye kanuni za usajili zitambana Mganda huyo.
Suala kama la Okwi ufafanuzi wake unaweza kupatikana katika kanuni ya tano ya usajili aya ya kwanza hadi ya tatu, ambao kwa muhtasari inasema mchezaji anaweza kusajili na klabu zisizozidi tatu kwa msimu, lakini ataruhusiwa kuchezea mechi za mashindano katika timu mbili tu.
Kama Okwi alicheza mechi za mashindano Etoile na akacheza pia na SC Villa ambazo ni pamoja na Ligi Kuu na vikombe, ina maana hawezi tena kuchezea Yanga SC mechi za mashindano.
Aya ya tatu ya kanuni hiyo inasema; “3. Players may be registered with a maximum of three clubs during one season. During this period, the player is only eligible to play official matches for two clubs,”.
Tafsiri yake; “Mchezaji anaweza kusajiliwa na klabu zisizozidi tatu kwa msimu, lakini katika msimu husika hawezi kuchezea mechi rasmi katika klabu zaidi ya mbili,”.
credit binzuberry