Saturday, 8 February 2014

CAF yaizuia leseni ya Okwi






STRAIKA wa Yanga, Emmanuel Okwi, hataichezea timu yake katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika leo Jumamosi dhidi ya Komorozine ya Comoro baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kushikilia leseni
yake.
Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba CAF imeshikilia leseni hiyo kutokana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutuma nakala ya barua yao iliyokwenda Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa)  kuomba ufafanuzi juu ya uhalali wa uhamisho wa Okwi wa kuichezea Yanga.
Mmoja wa maofisa wa TFF, alisema jana Ijumaa kuwa CAF imewapatia leseni za wachezaji wengine 25 kati ya majina 26 yaliyokuwa yametumwa na Yanga, huku leseni ya Okwi ikibaki Cairo, Misri.
“CAF wamesema kuwa wakipata ufafanuzi kutoka Fifa watatuma leseni hiyo, lakini kwa sasa hawataki kuleta mkanganyiko mwingine,” alisema ofisa wa TFF.
Mchezaji huyo ambaye awali alikuwa wa Simba, aliuzwa kwenda Etoile du Sahel ya Tunisia.
Hata hivyo inadaiwa kuwa klabu hiyo haikuilipa Simba na wala haikuwa ikimpa mshahara, jambo lililomfanya Okwi asuse na kurejea kwao Uganda kabla ya kuruhusiwa na Fifa kwa muda kujiunga na Villa ya Uganda kisha kuibukia Yanga