Thursday, 6 February 2014

ANGALIA PICHA ZA MTOTO WA MIAKA 7 ACHOMWA MIKONO NA MAMA YAKE MZAZI KISA MAYAI YA KUKU

 
Mtoto EMILLY GEORGE[7] Mkazi wa kijiji cha RUANDA wilaya ya Mbeya akilia kwa uchungu maumivu ya vidonda baada ya kuchomwa moto na mama yake mzazi kisa akidaiwa kuiba mayai ya kuku jamani ukatili gani huu?
 Mama mzazi wa mtoto aliyechomwa moto ELESIA MWASILE[41] akipelekwa kituoni na wanausalama
Hapa wanausalama na mama mzazi wa mtoto huyo wakielekea kumwona mtoto huyo katika hospitali ya Rufaa Mbeya
Baada ya kukamatwa mama huyo katili alkabidhiwa kwa Dawati la Polisi Jinsia na watoto chini ya Kiongozi wa Wilaya D\SSGT PUDENSIANA BAITU akimjulia hali mtoto Emilly
Wimbi la ukatili dhidi ya watoto bado limezidi kuchukua sura mpya baada ya mtoto EMILLY GEORGE[7] Mkazi wa kijiji cha RUANDA wilaya ya Mbeya kuunguzwa vibaya mikono yote miwili na mama yake mzazi ELESIA MWASILE[41] kwa maji ya moto kisha kufungiwa ndani kwa siku saba bila matibabu yoyote.

Akiongea huku akitetemeka kwa hofu ELESIA amesema kuwa chanzo cha cha kumchoma mtoto huyo ni kutokana na malalamiko ya majirani wakimtuhumu mtoto huyo kujihusisha na vitendo vya wizi vikiwemo wizi wa pesa na mayai ya kuku.

Tukio la mwisho lililopelekea mtoto huyo hadi kuchomwa ni pale ilipodaiwa na mama huyo kuwa mtoto aliiba mayai akidai amechoshwa na tabia za malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa jirani zake.

Baada ya kuunguzwa kikatili mtoto huyo alifungiwa ndani kwa siku saba bila matibabu yoyote hali iliyowafanya majirani kuuliza aliko mtoto kutokana na mtoto huyo kutoonekana mitaani hali iliyopelekea kutolewa taarifa ofisi ya kijiji ili kubaini aliko mtoto.

Uongozi wa kijiji baada ya kupata taarifa kwa majirani walifanya upekuzi na kumkuta mtoto amefungiwa ndani huku akiwa na majeraha makubwa katika mikono yote miwili ndipo taarifa ilitolewa kituo cha Polisi MBALIZI ambapo mama huyo alikamatwa.

Baada ya kukamatwa mama huyo katili alkabidhiwa kwa Dawati la Polisi Jinsia na watoto chini ya Kiongozi wa Wilaya D\SSGT PUDENSIANA BAITU na Mwenyekiti MARY GUMBO ambaye muda wote alikuwa akiangua kilio kutokana na kitendo alichofanyiwa mtoto na mama yake mzazi.

Hivi sasa mwanamke huyo anahojiwa na Polisi kituo kikuu cha kati na atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo na mtoto amelazwa katika Hospitali ya Rufaa wadi namba tano akiendelea kupatiwa matibabu.

Vitendo vya unyanyasaji vimendelea kukemewa Mkoani Mbeya na Asasi mbalimbali hasa kwa watoto vikiwemo vya ubakwaji,ulawiti,kazi za ndani na baadhi ya watoto wamepata ulemavu wa kudumu ikiwemo kupoteza viungo.