Msichana
mmoja, Mariam Chacha, mkazi wa Mtaa wa Nyasho A, mjini Musoma
amemwagiwa maji ya moto na kuunguzwa mwili, hali iliyofanywa alazwe
katika hospitali ya mkoa.
Tukio
hilo la kusikitisha lilitokea Oktoba 22 mwaka huu saa mbili usiku
ambapo inadaiwa aliyefanya kitendo hicho ni Pendo Wambura ambaye
amekamatwa na polisi.
Habari kutoka ndani ya kituo cha polisi mjini hapa zinadai kuwa mara baada ya Mariam kumwagiwa maji ya moto na mwenzake na kuungua
sehemu za kitovu mpaka usoni, matiti na mikono na akiwa hajitambui
mpaka sasa,wasamaria wema walimpeleka polisi ili kupata hati ya matibabu
(PF 3) na akaenda kutibiwa katika Hospitali ya Serikali ya Musoma
alikolazwa wodi namba nne.
“Polisi tulikwenda kumkamata
mtuhumiwa na tunamshikilia kwa kuwa majeruhi hali yake ni mbaya,
kalazwa, na tayari amefunguliwa jalada namba MUS/IR/5009/013,” alisema
afisa mmoja wa polisi kwa sharti la kutoandikwa jina lake kwa kuwa siyo
msemaji.
Shuhuda mmoja alimwambia
mwandishi wetu kwamba Mariam alikwenda kuwasalimia ndugu zake pamoja na
mama yake ambaye ni mgonjwa wanaokaa nyumba moja na mtuhumiwa.
“Mariam alipoona hali ya mama
yake alianza kulia ndipo Pendo alipokwenda kuchukua maji yaliyokuwa
yakichemka ili yapikiwe ugali wa mama mwenye nyumba na akamwagia
mwenzake akidai eti anachukizwa na kitendo chake cha kumlilia mgonjwa
wake,” kilisema chanzo.
-GPL