Monday, 23 December 2013

Simba wavuna milioni 60, Yanga wakosa mamilioni

Kikosi cha Simba.

KIKOSI cha Simba kitakomba Sh milioni 60 ambazo kiliahidiwa na uongozi wa timu hiyo iwapo kingeifunga Yanga katika mchezo wa Nani Mtani Jembe uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wakati Simba wakijiandaa kukomba kitita hicho baada ya kuwafunga watani wao mabao 3-1, Yanga wamekosa Sh milioni 60 ambazo uongozi wa Jangwani uliahidi kuwapa wachezaji kama wataifunga Simba zaidi ya mabao manne.

Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Sued Nkwabi, ameliambia Championi Jumatatu kuwa, uongozi wa timu yao kabla ya mchezo huo, ulionana na wachezaji na kuwaambia watapata Sh milioni 60 kama wakiifunga Yanga.
“Tumefurahishwa sana na kazi kubwa iliyofanywa na wachezaji wetu katika mchezo wa leo (juzi), walijituma kadiri ya uwezo wao kuhakikisha wanarudisha heshima ya timu yetu, kama tulivyowaahidi kabla ya mchezo kwamba, endapo watawafunga Yanga kwa idadi yoyote ya mabao tutawapatia fedha taslimu Sh milioni 60, ahadi hiyo tutaitekeleza mara moja,” alisema Nkwabi.
Wakati Simba hali ikiwa hivyo, mmoja wa mabosi wa Yanga ambaye hakupenda kutajwa jina, alisema: “Wachezaji wetu wametuangusha sana leo (juzi), kwanza tuliwaambia kama watashinda kwa ushindi wowote tutawapatia Sh milioni 40, lakini endapo wangepata mabao manne, kiasi hicho kingeongezeka kufikia Sh milioni 60.”