Monday, 3 March 2014

Tambwe apiga 19 Simba, Motema Pembe wamfuata





STRAIKA, Amissi Tambwe, wa Simba amefikisha mabao 19 katika Ligi Kuu Bara baada ya jana Jumapili
kuiwezesha timu yake kushinda mabao 3-2 dhidi ya Ruvu Shooting, huku klabu ya DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo, ikimpigia simu kutaka kumsajili haraka.
Katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting uliofanyika Uwanja wa Taifa, Tambwe ambaye ni raia wa Burundi, aliifungia Simba mara mbili dakika za 23 na 33.
Bao la kwanza alilifunga akimalizia mpira uliotemwa na kipa Abdallah Rashid wakati akiokoa shuti kali la Said Ndemla. La pili alilifunga pale alipounganisha krosi safi ya Haroun Chanongo.
Mabao hayo yanamfanya Tambwe kuvuka rekodi ya Boniface Ambani aliyefunga mabao 18 msimu wa 2010/11 alipokuwa Mfungaji Bora.
Bao la tatu la Simba katika mchezo huo uliohudhuriwa na watazamaji wachache huku mvua ikitawala muda mwingi, lilifungwa na Chanongo dakika ya 75 baada ya kupokea pasi ya Amri Kiemba.
Ruvu Shooting ilipata bao la kwanza dakika ya 68 lililofungwa na Said Dilunga kwa kichwa akiunganisha kona ya Michael Aidan. Bao la pili la Ruvu lilifungwa kwa njia ya penalti dakika ya 82 na Jerome Lembele.
Mwamuzi, Nathan Lazaro, wa Kilimanjaro alitoa penalti hiyo baada ya beki wa Simba, Joseph Owino, kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.
Licha ya ushindi huo, Simba imebaki katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 35 kwani Mbeya City ina pointi 36 katika nafasi ya tatu baada ya juzi Jumamosi kutoka suluhu na Oljoro JKT.
Baada ya mchezo huo, Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic alisema:
“Nimefurahi kupata ushindi huu, lakini nimefurahishwa zaidi na mabao tuliyofunga. Sasa naangalia michezo inayofuata.”
Naye Kocha wa Ruvu, Tom Olaba alisema: “Japokuwa napoteza mechi  pili mfululizo, nashukuru tumecheza na kupunguza idadi ya mabao ya kufungwa sasa natengeneza timu ya msimu ujao.”
Wakati huohuo,  DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imempigia simu Tambwe ikitaka kumsajili kwa msimu ujao wa Ligi Kuu ya nchi hiyo.
Tambwe aliliambia Mwanaspoti kuwa viongozi wa Motema Pembe walimpigia simu wakitaka ajiunge nao kwa msimu ujao na mazungumzo yao yanaenda vizuri kwani kilichobaki ni klabu hiyo kumalizana na Simba kwa kuwa bado ana mkataba na Wekundu wa Msimbazi hao.
“Nilipojiunga na Simba nilisaini mkataba wa miaka miwili, mwishoni mwa msimu huu nitakuwa nimemaliza mwaka mmoja hivyo Motema Pembe wanatakiwa kumalizana na Simba, mimi sina tatizo,” alisema Tambwe.
“Malengo yangu ni kucheza soka la kimataifa zaidi, sijaridhika na hapa nilipo, tayari ndoto zangu zimeanza kutimia kutokana na Motema Pembe kuonyesha nia ya kunisajili.”