Wakati
zikiwa zimebakia takribani siku tano kabla ya wawakilishi wa Tanzania
bara katika michuano ya kombe la CAF Champions League - Dar Young
Africans kuwavaa mabingwa watetezi Al Ahly katika dimba la Cairo Stadium
uliopo ndani ya mji mkuu wa Misri, Cairo, mtandao huu utakuwa
unakuletea namna gani klabu ya Simba - mahasimu wa Yanga walivyoweza
kuvunja rekodi na kuivua ubingwa Zamalek.
Simba
walishinda 1-0 katika mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam,
Yanga nao pia wameshinda 1-0 dhidi ya wapinzania wao. Kinadharia
inaonekana Yanga wana nafasi ya kuvuka kwenda hatua ya mbele kwa sababu
tayari wameshapata ushindi nyumbani, ingawa rekodi yao katika viwanja
vya timu za kiarabu sio nzuri. Ila pamoja na haya Yanga bado wanaweza
kuiondoa kwenye michuano Al Ahly. Simba waliweza hata pia Yanga inaweza,
ila kwa mbinu gani. Swali ni kwa namna gani wataweza kupata matokeo
chanya jumapili ijayo dhidi ya Al Ahly.
Mtandao
huu unakuletea mahojiano na katibu mkuu wa zamani wa Simba Kassim
Dewji, akielezea namna ambavyo Simba na watanzania kwa umoja wao
walivyoiwezesha klabu hiyo ya msimbazi kuvunja rekodi na kuitoa Zamalek
ndani ya ardhi yao.
"Kwa
kawaida kwa wakati huo ndege inapotoka Dar hupitia Nairobi kisha
Khartoum then Cairo. Kwenye ndege tulikuwa viongozi, wachezaji pamoja na
wazee wa kamati ya ufundi. Mzee mmoja wa kamati ya ufundi alituambia
lazima ili vitu vikae sawa lazima tufike Cairo kwenye muda aliotupangia,
sisi kama viongozi tulishajua kwamba suala lile halitowezekana kwa
sababu ndege lazima ingepita Khartoum - Sudan kwanza hivyo tusingefika
Cairo muda aliotaka, tulipomwambia hivyo akasema tumuachie yeye atajua
cha kufanya na tungefika Cairo muda uliotakiwa.
"Tulipokuwa
tunakaribia Khartoum, pilot alipokuwa akifanya mawasiliano na wenzake
uwanja wa ndege wa Khartoum akaambiwa hali ya hewa ni mbaya sana, mpaka
tunafika Khartoum pilot alishindwa kuuona hata uwanja wenyewe na hivyo
ikamlazimu kupeleka ndege moja kwa moja mpaka Cairo na tukafika muda ule
ule aliotaka yule mtaalam."
"Tangu
tunafika kule wote tulikuwa tunajua hila na karaha za wapinzani wetu
hivyo tulijidhatiti kukabiliana na hali yoyote ya kutoodhofisha. Uwanja
ndege tuliposhuka kwa sababu kuna wenzetu walikuwa wameshatangulia hivyo
walikagua basi tuliondaliwa na kulisafisha kwa kila namna kuhakikisha
lilikuwa na usalama. Tuliondoka na kuelekea kwenye hoteli
waliyotuandalia.
HOTELINI - CHAKULA
"Tulipofika
hotelini tukavifanyia uchunguzi vyumba vyote, tukaridhika tukawaruhusu
wachezaji waingie vyumbani. Vyakula vya wachezaji tulikuwa tunapika
wenyewe na vyakula vya hotelini tulikuwa tunakula viongozi, wadau na
mashabiki tulioenda nao Misri.
"Wakati
tunajiandaa kulala wachezaji wote wakiwa wameshaingia vyumbani kwao,
mie nikiwa chumbani kwangu nikawasha TV nikakuta zimeongezwa TV stations
kadhaa zinaonyesha filamu za ngono. Nilipoona vile nikajaribu kuanza
kupiga simu kwenye kila chumba, nikashangaa kuona simu inapokelewa mara
1, hivyo nikagundua wachezaji walikuwa macho wanaangalia ule ujinga, na
muda huo ilikuwa saa 7 usiku. Baada ya kugundua hilo jambo niliwafuata
viongozi wenzangu tuliokwenda nao na tukajadili lile suala na kuona
lilikuwa limefanyika kusudi na uongozi wa hoteli ili kuwafanya wachezaji
wasilale mapema na kuwahamasisha kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu,
ukizingatia kwenye ile hoteli juu kabisa na chini kwenye basement
kulikuwa na kumbi za starehe hivyo walikuwepo madada poa.
Aliyekuwa katibu mkuu wa Simba Kassim Dewji
"Hivyo tulikubaliana na viongozi wenzangu kwamba tuhame hotel ili kuepeukana na mambo yale. Zamalek walipokuja Dar tuliingia contract ya kuwapa hotel waitakayo hapa Dar na wenyewe kutupa hotel tutakayotaka kule Cairo. Hivyo nasi tulipokuwa hatujaridhika na hotel waliyotupa tuliwataarifu na mwanzoni waligoma kubadilisha, lakini kwa sababu mkataba ulikuwa unawabana, ikabidi wakubali kutubadilishia.
"Hivyo tulikubaliana na viongozi wenzangu kwamba tuhame hotel ili kuepeukana na mambo yale. Zamalek walipokuja Dar tuliingia contract ya kuwapa hotel waitakayo hapa Dar na wenyewe kutupa hotel tutakayotaka kule Cairo. Hivyo nasi tulipokuwa hatujaridhika na hotel waliyotupa tuliwataarifu na mwanzoni waligoma kubadilisha, lakini kwa sababu mkataba ulikuwa unawabana, ikabidi wakubali kutubadilishia.
"Wachezaji
wote wakahama pale hoteli na baadhi ya viongozi, wakaenda kukaa kwenye
apartments. Viongozi na mashabiki wengine walibakia pale hotelini. Uzuri
wa kuhamia kule kwenye apartments, ambazo kila moja ilikuwa na vyumba
vitatu - ilikuwa rahisi kuwasimamia wachezaji. Kwenye apartment walikaa
wachezaji wawili na kiongozi mmoja. Vyakula tuliendelea kupika wenyewe.
KUKATAA OFA YA SHOPPING NA KUPELEKWA KUONA PYRAMID
"Zamalek
walikuwa na kila aina ya mbinu katika kuhakikisha wanawatoa wachezaji
katika kuweka umakini kwenye mchezo. Walikuja na kutueleza kwamba
watupeleke shopping tukawajibu kwamba hatukuwa na fedha za kufanya
shopping, wakatupa ofa ya kumfanyia shopping kila mmoja wetu.
Tukawaambie tungekwenda lakini kwa sasa concentration yetu ilikuwa
kwenye kujiandaa na mechi. Pia walitupa ofa ya kutupeleka kuona Pyramid,
tukawapa ahadi ya kwenda siku kadhaa mbele.
"Siku moja kabla ya
mechi wakati tukitoka mazoezini dereva wa basi akaanza kutupeleka kwenye
shopping mall, tulipostukia tukalamzisha apeleke gari hotelini.
ULINZI NA USHIRIKIANO
"Moja ya vitu
vilivyochangia kwa asilimia fulani kuweza kuwatoa Zamalek ulikuwa ni
ushirikiano wa Simba kama timu, taasisi, wadau wa soka, na watanzania
kwa ujumla. Viongozi wote tulienda, Friends of Simba almost wote
walikuwa kule, watanzania wengine ambao sio washabiki wa Simba kama
akina Dr Ramadhan Dau (Pan African), Godfrey na Joseph Kusaga nao
walijumuika nasi kule Cairo kuhakikisha ushindi unarudi Tanzania.
"Mdhamini wetu mkuu
kupitia kampuni ya Mohamed Enterprises, Mohamed Dewji alikuwa nasi bega
kwa bega siku zote tulizokuwa Cairo.
"Tulikuwa tunagawana
zamu za kulinda kila kitu, wakati wa mazoezi viongozi wengine tulienda
na timu, wengine walibaki kuhakikisha kuna usalama katika vyumba
tulivyofikia.
"Waziri wa michezo wakati huo Juma Kapuya na wazira yake kwa ujumla walitupa ushirikiano wote tuliohitaji."
SIKU YA MECHI - UWANJANI
"Siku ya mechi kabla
hatujaondoka hotelini tuliongea na wachezaji kuwapa moyo na kuwaweka
sawa kisaikolojia. Mdhamini wetu Mohamed Dewji alitoa ahadi ya kiasi cha
fedha kizuri kwa wachezaji endapo wangeshinda. Hivyo wachezaji walikuwa
na kila aina ya sapoti waliyohitaji. Watanzania kadhaa nyumbani na kule
ugenini walikuwa wakituombea dua na kheri ya ushindi.
"Tuliwahi kufika
uwanjani masaa matatu kabla ya mchezo kuanza, lakini hatukuingia
vyumbani. Viongozi kwa kushirikiana na wadau wengine tulienda kukagua
dressing room, tulipiga deki na kuhakikisha hakukuwa na mchezo wowote
mchafu uliofanyika dhidi yetu.
"Tuliingia vyumbani
wakati wa kwenda kukaguliwa tu na refa kwa sababu ilikuwa ni sheria,
lakini wakati huo tulikuwa tumeshajiridhisha chumba kilikuwa kisafi.
Wakati tunaelekea uwanjani, Crescentus Magori aliamua kubaki chumbani
ili kulinda Zamalek wasije kufanya michezo yao ya kupuliza madawa ndani
ya vyumba ambayo huwachosha wachezaji, Magori alikaa mpaka tuliporudi
mapumziko. Kipindi cha pili ndio tukaenda nae uwanjani kwa sababu
Zamalek wasingeweza kufanya chochote kwa kuwa hatukuwa tunarudi tena
uwanjani baada ya kipindi cha pili."
UBORA WA TIMU
"Hayo yote
tuliyoyafanya yalikuwa asilimia 20 tu, asilimia 80 zilizobaki zilibaki
uwanjani kwa wachezaji. Kwa hakika Simba ilikuwa na timu bora, kocha
bora na uongozi bora. Siang'a alikuwa kocha mshindani ambaye hakupenda
kufungwa, kwa ushirikiano wetu sote ndio maana tukafanikiwa.
"Wachezaji walijituma
sana pamoja na vitendo vya refa lakini hawakukata tamaa walijitahidi na
kufanikisha kazi iliyowapeleka uwanjani.
USHAURI KWA YANGA
"Yanga wana timu
nzuri, wanachopaswa kujituma na kupanga vizuri. Lazima kuwe na
ushirikiano mkubwa ndani ya timu, kwa wachezaji, benchi la ufundi,
viongozi na mashabiki kwa kushirikiana na watanzania wote pasipo kujali
itikadi za timu.
"Serikali pia inabidi
nayo iwape ushirikiano mkubwa Yanga. Viongozi waache kutafuta sifa
binafsi, umoja ni kitu muhimu, timu inapofanya vizuri kila mtu atapata
sifa yake."


