Beki kisiki wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani.
Sweetbert Lukonge na Hans Mloli UPEPO mbaya ambao unaendelea ndani ya Yanga, ambayo makao makuu yake ni Jangwani jijini Dar es Salaam, hasa juu ya wachezaji wa timu hiyo ambao sasa umefika mpaka kwa wazazi wa wachezaji wa timu hiyo.
Baba wa beki Kevin Yondani, mzee Patrick Yondani, ameingilia kati suala hilo, huku baba wa straika Jerry Tegete, mzee John Tegete, naye akitoa neno juu ya mwanaye huyo ambapo kwa pamoja wamezungumza kwa hisia kali.
Yondani anatuhumiwa kufungisha katika mechi dhidi ya JKT Mgambo ya Tanga, ambapo mzee Yondani amewataka viongozi wa Yanga kuacha kumshutumu mwanaye kwa kusema kucheza chini ya kiwango huwa inatokea kwa mchezaji yeyote na kuwataka kuacha kumsakama mwanaye.
Yanga ilifungwa mabao 2-1 katik mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Jumapili iliyopita, ambapo Yondani alikuwa mmoja wa wachezaji waliohusishwa kupewa fedha ili waisaliti timu yao hiyo, lakini mzee Yondani anapinga hilo kwa nguvu zote.
Akizungumza na Championi Jumamosi, mzee Yondani alisema hakubaliani kabisa na tuhuma kuelekezwa kwa mwanaye kwa kuwa anajua hawezi kufanya hivyo.
“Timu zetu hizi hususani Simba na Yanga zina matatizo makubwa, zinamthamini mchezaji anapofanya vizuri lakini anapofanya kosa zinamgeuka na kuwa adui, mpira hauko hivyo, kama ungelikuwa hivyo basi wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa Ulaya wangelikuwa wanatuhumiwa kila siku.
“Wanasahau Yondani kawafanyia mambo mengi mazuri na kuiletea sifa klabu hiyo lakini leo hii kwa sababu kafanya kosa moja wanamgeuza adui, hakika hali hiyo imenisikitisha na siyo ya kimichezo.
“Nawaomba wanaofanya hivyo wawe wanafuatilia soka la nje, watajifunza mambo mengi. Nimeshazungumza na Yondani, ameniambia hakucheza chini ya kiwango na wala hakuchukua fedha zozote ili aisaliti timu,” alisema mzee Yondani.
Katika hatua nyingine Yondani ataukosa mchezo wa kesho dhidi ya JKT Ruvu ambao utafanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar kutokana na kuwa na kadi tatu za njano.
Wakati huohuo, mzee Tegete ambaye mwanaye yupo kwenye wakati mgumu kutokana na kutokuwa na namba ya uhakika kwenye kikosi cha kwanza, amesema mwanaye anafanyiwa fitina klabuni hapo kwa kusingiziwa kiwango kimeshuka ilimradi wampoteze kwenye ramani ya soka Tanzania.
“Si kweli kabisa kwamba mwanangu ameshuka kiwango ila basi tu, ni kama hana bahati au pengine anafanyiwa majungu kwa sababu sidhani kama kuna straika Tanzania mwenye kiwango kama chake, nazungumza haya nikiwa kama kocha pia.
“Ukiacha hao wanaotoka nje hakuna mtu mwenye kipaji cha kufumania nyavu zaidi yake, we fikiria ndani ya mechi saba alizoichezea Yanga msimu huu amefunga mabao sita, sasa mtu unataka kuwa na mchezaji mwenye kiwango cha aina gani ndiyo uridhike?
“Kutokana na kuwekwa benchi pale Yanga kumemfanya hata timu ya taifa, Taifa Stars, haitwi sasa. Ni bora ahame timu aende akacheze hata Msumbiji au nchi nyingine tu pengine akienda huko anaweza akanufaika zaidi kisoka.