Na Hans Mloli
KOCHA Mkuu wa
Yanga, Hans van Der Pluijm, amewashtukia Al Ahly na kukiri kwamba
waliwadanganya Yanga kwa kudai watakuja na winga wao Emad Motaeb, lakini
haikuwa hivyo.
Al Ahly ilitoa taarifa mbalimbali kwenye vyombo vya habari vya Cairo
kwamba itatua na winga wao hatari Motaeb jijini Dar es Salaam kwa ajili
ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Yanga lakini haikuwa
hivyo.
Pluijm amecharuka na kusema anajua kwamba, Ahly walitangaza kuja na
winga huyo ili kuwatisha Yanga, lakini wameamua kumuacha kwa ajili ya
mchezo wa marudiano utakaochezwa Jumapili ijayo kwa kuwa wameweka nguvu
zaidi kwenye mchezo huo wa pili.
Hata hivyo, Pluijm ameliambia Championi Jumatatu kuwa, hawajatishika
na hilo na kikosi chake kinajiandaa kwenda Misri kupambana ili kuibuka
na ushindi.
Ingawa Pluijm amekiri kwamba Motaeb ni hatari na ni mwepesi anapokuwa uwanjani linapofika suala la kushambulia.
“Wale ni wajanja, nazijua mbinu zao, huenda wakabadilika kwenye
mchezo wa marejeano, inabidi kujiandaa kwa kila kitu kwa sababu sidhani
kama watacheza hivi kwa staili hii waliyoitumia leo.
“Hata hivyo,
kuna mchezaji mmoja sijamuona na yupo kwenye timu yao, ni hatari sana,
mara nyingi huwa anacheza winga, simjui jina lake sawasawa, najaribu
kulikumbuka jina lake lakini linanitoka ila namfahamu kwa staili yake ya
uchezaji,” alisema Pluijm na kuongeza:
“Hata hivyo haimaanishi kwamba tukienda kule tutazuia tu, hapana
tutacheza kwa kushambulia kwa sababu tunahitaji ushindi, bado tunahitaji
mabao kwa ajili ya kujihakikishia kuvuka raundi hii.”
Uchunguzi
uliofanywa na Championi Jumatatu umegundua kuwa mchezaji aliyesemwa na
Pluijm ni Motaeb ambaye ni mmoja wa wachezaji hatari kwenye kikosi cha
Al Ahly na huvaa jezi namba tisa mgongoni.
Mbinu nyingine iliyoonekana kutumika na Waarabu hao ni ile ya
kumbadili namba mchezaji wao, Sayed Abdel Wahed ambaye hutumika kwenye
nafasi ya kiungo mshambuliaji lakini juzi alionekana kupewa majukumu ya
beki wa kushoto.
Yanga itakwenda Misri kurudiana na Al Ahly Jumapili ijayo, baada ya
kupata ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, juzi.