YANGA wamemshitua straika wa Simba, Amissi Tambwe baada ya kumzingira, kuonyesha hisia zao kwa makali yake ya kucheka na nyavu halafu wakampooza na buku 10 akabaki anacheeka huku mashabiki wa timu yake wakiingiwa hofu.
Mashabiki hao walifanya tukio hilo baada ya mechi
ya Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa
juzi Jumapili, baada ya mchezaji huyo kufunga mabao mawili Simba
ikishinda 3-2.
Mabao hayo yalimfanya Tambwe kutimiza mabao 19
kwenye msimamo wa wafungaji ambapo ameweka rekodi ya aina yake kwani
katika miaka ya hivi karibuni hakuna mchezaji aliyefikisha mabao hayo.
Mashabiki hao waliosimama upande wa Jukwaa la
Yanga, mechi hiyo ilipomalizika walipiga kelele wakiita jina la Tambwe
ili wazungumze naye jambo na kumpongeza kwa makali yake na
alivyowafuata walimgombania na mmoja wao akampa buku 10 (Sh 10,000)
akainyaka akaishia zake nje ya uwanja.
Mchezaji huyo aliwaacha mashabiki hao
wakijadiliana huku wakionekana kufurahishwa na akili ya kuona goli
aliyonayo straika huyo. Tambwe alipofuatwa na Mwanaspoti baada ya
kuachana na mashabiki hao alionyesha kushangazwa na walichomfanyia Yanga
kwani hakutarajia lakini hakutaka kuingia kiundani kwa kuhofia inaweza
kumletea matatizo kwa viongozi wake na mashabiki.
Tambwe alisema: “Nashukuru na nafikiri wamevutiwa
na mimi, siwezi kuzungumzia zaidi.” Pamoja na kucheza vizuri kwenye
mchezo huo, Zdravko Logarusic alimtoa kwenye mechi hiyo zikiwa zimebaki
dakika 18 na akasema alifanya hivyo kwa ajili ya kumlinda.
“Unajua nafanya hivi kwa sababu uwezo wake wa
kufunga mabao mengi huwa ni kero kwa mabeki wa timu pinzani ambao huwa
wanamwinda ili wamuumize na ndivyo nilivyoona, ndiyo maana nikamtoa,”
alisema Logarusic.
“Si unajua kama watafanikiwa malengo yao ya
kumuumiza akakaa nje atakuwa ameigharimu timu, Tambwe ni mchezaji mzuri
na muhimu kwenye timu ukimkosa ni hatari.”
Awaambia mashabiki Simba
Tambwe amesema kitendo cha mashabiki kumshangilia
yeye pekee baada ya mechi si kizuri kwani kinaweza kuigawa timu hiyo
kongwe nchini. Katika mechi dhidi ya JKT Ruvu na Ruvu Shooting
zilizochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Saalam, Tambwe alipokewa kwa
shangwe na mashabiki wa Simba hadi lango kuu la kutokea uwanjani hapo
ambapo huchukua bajaji na kuondoka.
Akizungumzia suala hilo Tambwe alisema, “Unajua ni
vizuri kumpongeza mtu anapofanya vizuri ila pia mashabiki wanapaswa
kukumbuka kuwa mimi si kitu nikiwa peke yangu, hii ni timu na mimi ni
mfungaji tu.”
“Mashabiki wanapaswa kuelewa kuwa bila kazi kubwa
inayofanywa na wachezaji wengine mimi nisingeweza kufunga, hivyo
waishangilie timu kwa ujumla,” aliongeza Tambwe.
“Nina malengo ya kucheza soka la kulipwa nje ya Afrika Mashariki
na pengine nje ya Afrika lakini unapotaka dili zikuangukie lazima uwe
na kitu fulani tayari umeshakifanya hivyo kama straika ninahitaji kuwa
na mabao ya kutosha.”
“Mimi kwa michezo sita iliyobaki nataka
kuhakikisha, mitatu ijayo ninapata mabao sita na hiyo michezo mingine
itakayosalia ni mipango ya Mungu tu.
“Nina mabao 19 na nikifikisha 25 nitakuwa
nimejitangaza vya kutosha na kuzikaribisha timu nyingine kwa ajili ya
kufanya kazi na mimi. Ninavyoongea na wewe DC Motema Pembe ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo inanihitaji,” alisema.