Mmoja wa
manusura wa mauaji ya maangamizi ya Rwanda ya mwaka 1994 akíwaombea
wahanga wa mauaji mbele ya mafuvu yao katika kaburi la pamoja la
Nyamata.
Umoja wa
Mataifa umewasha mwenge kuzindua mkururo wa matukio yaliyopangwa
kufanyika kwa nia ya kukumbuka miaka 20 ya mauaji ya maangamizi ya mwaka
1994 nchini Rwanda ambapo zaidi ya watu 800,000 waliuawa.
Akizungumza
jijini New York katika kile kilichopewa jina la "Kwibuka 20", Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, alisema miaka 20 baada ya mauaji
hayo ya maangamizi, kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kuzuia maafa
nchini Syria ni jambo la aibu. Idadi ya washaopoteza maisha hadi sasa
nchini Syria ni 140,000 kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Hata
hivyo, Ban Ki-moon ameusifu uwezo wa Rwanda kuungana na kupatanisha
baada ya mkasa huo na kusema umekuwa kivutio. Mauaji ya Rwanda yalianza
masaa machache baada ya ndege iliyokuwa imembeba Rais Juvenal
Habyarimana kuangushwa wakati ikikaribia mji mkuu, Kigali, tarehe 6
Aprili 1994.
Ndani ya
siku 100 baada ya hapo, mauaji dhidi ya jamii ya Kitusti na Wahutu wenye
msimamo wa wastani yaliangamiza roho za watu wapatao laki nane.
Wakati
huo Umoja wa Mataifa ulikuwa na kikosi kidogo cha walinda amani nchini
Rwanda, lakini Baraza la Usalama lilikataa kuongeza askari zaidi
kukabiliana na mauaji hayo ya maangamizi, na hata nchi moja moja
hazikutoa msaada wowote.
Syria kama Rwanda?
Hali
inaonekana kufanana na hiyo kwa mauaji ya Syria, ambako hadi sasa bado
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limegawika vibaya juu ya mgogoro
huo, ingawa Jumamosi iliyopita lilikubaliana kwa kauli moja juu ya
azimio linaloyaruhusu mashirika ya misaada kuingia kwenye maeneo
mbalimbali nchini humo.
Katika
halfa hiyo ya hapo jana, Ban Ki-moon alisema licha ya Umoja huo
kujifunza namna ya kuzuia maafa kama ya Rwanda, lakini hakuna uhakika
kwamba matukio kama hayo hayawezi kujirejea.
"Mauaji
ya maangamizi nchini Rwanda yalikuwa ni ishara kubwa ya kushindwa kwa
jamii ya kimataifa kuchukua hatua dhidi ya uhalifu mbaya kabisa. Tunajua
vyema zaidi sasa kuliko hapo kabla kwamba mauaji ya maangamizi si tukio
moja tu, bali mchakato unaojumuisha mambo kadhaa na muda mrefu."
Alisema Ban Ki-moon.
Ulaya nako kwatajwa
Mkuu huyo
wa Umoja wa Mataifa alizungumzia pia kupanda kwa kiwango cha chuki
dhidi ya wahamiaji, Waislamu na jamii ya Waroma barani Ulaya na pia
uvunjwaji mbaya kabisa wa haki za binaadamu katika Jamhuri ya Afrika ya
Kati.
Umoja wa
Mataifa unajaribu sasa kukabiliana na mauaji yanayochochewa kidini
kwenye Jamhuri hiyo ya Afrika ya Kati, lakini hali inatajwa kuwa mbaya.
Wiki
iliyopita, Ban Ki-moon alitoa wito wa kutumwa haraka kwa wanajeshi na
polisi 3,000 ili kusaidiana na walinda amani 6,000 kutoka Umoja wa
Afrika. Tayari wanajeshi 1,6000 wa Ufaransa wako huko, na Umoja wa Ulaya
umeahidi kutuma wengine 500.
Chanzo, dw.de/swahil