![]() |
| Watu wa kazi; Okwi kulia akiwa na Kiiza, tayari wapo Zambia kuitumikia timu yao ya taifa ya Uganda |
Tuesday, 4 March 2014
OKWI NA KIIZA TAYARI WAPO ZAMBIA NA THE CRANES, WATAONDOKEA HUKO KWENDA CAIRO
WASHAMBULIAJI
Waganda wa klabu ya Yanga SC, Emmanuel Okwi na Hamisi Kiiza wamewasili
jioni hii mjini Ndola, Zambia kujiunga na timu yao ya taifa, Uganda, The
Cranes kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa Jumatano dhidi ya
wenyeji Chipolopolo.
Okwi
na Kiiza ambao waliichezea Yanga SC Jumamosi ikiifunga Al Ahly ya Misri
bao 1-0 katika mchezo wa kwanza kuwania kutinga Hatua ya 16 Bora Ligi
ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Taifa, Dar ves Salaam waliondoka leo
nchini.
Kocha
Mserbia, Milutin Sredojevic ‘Micho’ ameiambia BIN ZUBEIRY jioni hii
kutoka Ndola kwamba wachezaji hao wamefika salama na wataichezea The
Cranes Jumatano kabla ya Alhamisi kwenda Cairo kuungana na klabu yao kwa
ajili ya mchezo wa marudiano na Al Ahly.
Kikosi
cha Yanga SC kilichoingia kambini leo hoteli ya Bahari Beach kujiandaa
na mchezo wa marudiano na Al Ahly, kinatarajiwa kuondoka Dar es Salaam
Alhamisi usiku kwenda Cairo.
Uongozi
wa Yanga SC ulijaribu bila mafanikio kumshawishi Micho aliyewahi
kuifundisha klabu hiyo mwaka 2007 awaache wachezaji hao waendelee na
maandalizi ya pamoja na wenzao kwa ajili ya mechi na Ahly.
Lakini
Micho amewaahidi Yanga SC atahakikisha yeye mwenyewe wachezaji
wanaondoka mara tu baada ya mechi hiyo iliyo katika kalenda ya
Shirikisho la Soka la Kimtaifa (FIFA).
