MANCHESTER, ENGLAND
KULIKUWA na kikao kwenye chumba maalumu cha mikutano ofisini kwa Edward Woodward huko Old Trafford, mara simu ikasikika ikiita.
Ulikuwa usiku wa nusu fainali ya Kombe la Ligi,
Manchester United ilipomenyana na Sunderland na kupoteza kwa mikwaju ya
penalti. Hilo lilikuwa pigo jingine kubwa kwa Man United katika msimu
huu.
Ndani ya chumba hicho kilichokuwa kikijadiliwa ni
uhamisho wa kiungo Mhispaniola Juan Mata. Mambo yalikuwa bado magumu,
hawakuwa wamempata staa huyo ambaye huenda akawasaidia kwenye nusu
fainali hiyo.
Hata hivyo, mazungumzo ya kumnasa Mata kutoka
Chelsea yalikuwa kwenye hatua nzuri. Woodward alionekana kuwa na
shughuli nyingi sana kwenye kulikamilisha suala hilo na hivyo kuacha
kunywa kahawa yake iliyokuwa kwenye kikombe mezani alipoketi.
Tangu alipochukua nafasi ya kuwa Mkurugenzi Mkuu
wa Manchester United, Woodward amekuwa akifanya mikutano ya mara kwa
mara na waandishi wa habari ofisini kwake. Ni mtu anayeonekana kutaka
kila anachokifanya kipate kutambulika kwa haraka.
Kwa utendaji wake wa kazi, huwezi kufikiria kama Man United inaweza kuzama wakati huo akiwa madarakani.
Siri yafichuka
Man United inaonekana kufanya mikakati ya usajili
wa kimyakimya. Kwenye mkutano huo, ndipo siri ya usajili wa Mata
ilipofichuka rasmi. Kwenye majira yajayo ya kiangazi, Man United
imepanga kufanya usajili wa nyota wa maana ili kukifanya kikosi hicho
kuwa na nguvu zaidi na kurejea kwenye makali yake.
Man United kwa sasa inashika nafasi ya saba kwenye
msimamo wa Ligi Kuu England jambo ambalo limekuwa likiwasumbua wadau
wake wengi wakiwamo mabosi wa klabu hiyo kwa sasa kufanya vibaya
kunaingia hasara kubwa klabu.
Ofisini kwa Woodward ndipo kulikofahamika siri
nyingi zinazohusu mipango ya klabu hiyo katika biashara za kufanya
usajili wa maana baada ya msimu kumalizika, lakini kubwa likitegemea
zaidi nafasi itakayoshika klabu kwenye ligi mwisho wa msimu.
Akiwa kwenye kikao hicho, mara simu yake iliita na kuwaomba
samahani waandishi waliokuwa mbele yake kwamba anapokea simu. Kwa bahati
mbaya, simu hiyo aina ya BlackBerry, ilijibonyeza spika ya nje kimakosa
na hivyo mazungumzo ambayo yangekuwa ya siri yaliweza kusikika bayana.
Sauti ya mtu aliyekuwa akipiga simu ikasikika na
wote waliokuwa kwenye mkutano huo na kufichua biashara za siri
zinazofanywa na klabu hiyo katika mipango ya kujiimarisha zaidi.
Woodward alishituka sana baada ya kugundua simu
yake inasikika. Kwa mshituko huo huo akamwambia aliyekuwa akizungumza
naye. “Tafadhali, subiri, acha usizungumze kitu.” Kisha alichukua simu
yake na kukimbilia kwenye chumba kingine na hapo akaponyeza kitufe cha
kuondoa spika ya nje ili kuficha siri.
Hata hivyo, presha hiyo ilibainisha wazi jinsi
bosi huyo alivyo kwenye wasiwasi mkubwa kutokana na mwenendo mbaya wa
kikosi cha Man United msimu huu.
Imefichuliwa kwamba kinachomtokea Woodward kwa
sasa kilimtokea pia mtangulizi wake, David Gill. Biashara zozote
haziwezi kwenda vizuri kama timu inapokuwa kwenye nyakati ngumu na
kupata matokeo mabovu kama ilivyo kwa sasa.
Usajili wa Mata
Man United ilipaniki na kuona hakuna namna
nyingine ya kuweka sawa msimu wao pengine zaidi ya kumsajili Mhispania
huyo. Walizama mfukoni na kumfanya staa huyo kuweka rekodi ya uhamisho
kwenye kikosi chao baada ya kumnasa kwa pauni 37 milioni kutoka Chelsea.
Lakini, usajili wa staa huyo ulikuwa wa mipango
zaidi kwa sababu ilikuwa sehemu ya kupanua soko lao la kibiashara na
kuongeza mauzo ya jezi baada ya kuona mambo yanaharibika kwenye upande
wa matokeo ya timu kwenye mechi zake.
Mastaa kama Robin van Persie, Wayne Rooney na
Marouane Fellaini, mauzo ya jezi zao yamekuwa si ya kasi sana kama
ilivyokuwa mwanzoni na hivyo waliamini usajili wa Mata unaweza kuwa na
kitu tofauti za kuzungumziwa katika klabu hiyo.
Hata hivyo, Mata ni mwanzo wa mipango ya usajili
wa nyota wengine watakaofuata Old Trafford baada ya mambo kufahamika
hadharani kwenye kikao hicho.
Ziara ya Dubai
Woodward alitengeneza mazingira ya kuipeleka timu
mapumziko Dubai kwenda kufanya mazoezi kwenye mazingira ya hali ya hewa
ya joto. Uamuzi wa kumbakiza Rooney kikosi hapo kwa pesa nyingi
ulifikiwa kwa ajili ya mtazamo wa kibiashara zaidi.
Kwenye ziara yake ya Dubai, Man United ililenga kwenye wigo wa
kibiashara ukiwa ni mpango wa kuweka mazingira sawa ya kucheza mechi za
kirafiki katika ukanda huo kama sehemu ya kuingia pesa kufidia hasara
itakayopata timu kutokana na kushindwa kuingia kwenye nne bora na
kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Tayari Man United imeshawanasa wadhamini kadhaa
ambao watawezesha kucheza mechi maalumu za kibiashara wakati
itakaposhindwa kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao na kwamba watakuwa
wakitembelea sehemu mbalimbali kuzunguka dunia kwa ajili ya mechi
maalumu kitu ambacho kinadaiwa kunaweza kuzishawishi klabu nyingine
kuingia kwenye mpango huo.
Matokeo mabovu ya uwanjani si kosa la Moyes wala
Woodward, lakini katika harakati za kupambana na presha ya kuingia
hasara uamuzi wa kucheza mechi za kirafiki zenye malipo ulifikiwa kama
timu itafeli kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Kwa nini Ferguson alishinda
Kwenye klabu ya Man United, Ferguson alikuwa
mjanja sana. Aliwafanya wachezaji wa timu hiyo kuwa sehemu yake. Man
United haikuwa na wachezaji tishio sana, lakini Ferguson aliwafanya
kupambana kwa ajili yake wanapoingia uwanjani. Kitu ambacho alikifanya
Mskochi huyo ni kwamba wachezaji wote aliowasajili alihakikisha
wanawafahamu vizuri hadi familia zao.
Amekuwa akiwatembelea wazazi wa wachezaji wake na
wakati mwingine kunywa nao chai kwenye makazi yao bila ya kujali kwambe
yeye ni mtu mashuhuri.
Mfano mzuri alikwenda nyumbani kwa kiungo Darren
Fletcher na kupata chakula pamoja na familia hiyo kwenye makazi yao ya
hadhi ya chini huko Edinburgh. Ferguson aliifanya Man United kuwa mali
yake, alimchagua kaka yake, Martin kufanya shughuli za kutafuta
wachezaji.
Jambo hilo na staili yake ya kuishi na wachezaji
ilifanya Man United kuwa klabu maarufu sana na kupata hadhi kubwa
duniani na hivyo kupata mikataba mbalimbali ya kuvutia wadhamini.
Lakini, ukweli halisi kama asingekuwa Ferguson, huenda Man United
ingekuwa klabu maskini sana.
Kitu ambacho anapaswa kukifanya Moyes ni kuiga
staili ya mtangulizi wake na kuwafanya wachezaji wake kucheza kama ndugu
kama ilivyokuwa enzi za Ferguson kitu ambacho alikifanya na kufanikiwa.
Ni aibu, kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya
uliofanyika Jumanne iliyopita dhidi ya Olympiakos, Van Persie alimpasia
mpira Rooney mara moja tu, jambo ambalo limeonyesha bayana kwamba
ushirikiano wa wachezaji hao ndani ya uwanja si mzuri.