Ngassa aliweka rekodi ya kufunga ‘hat trick’ mbili katika mechi mbili za
hatua ya awali dhidi ya Komorozine de Domoni ya Comoro ambayo Yanga
waliipata ushindi wa jumla ya mabao 12-2.
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Mrisho Ngassa bado
anashikilia rekodi ya kufunga ‘hat trick’ mbili kwenye mechi za Ligi ya
Mabingwa Afrika baada ya mechi za hatua ya kwanza ya michuano hiyo
kushindwa kupata‘hat trick’ yoyote.
Michezo 16 ya Ligi hiyo ilichezwa wikiendi
iliyopita ikishuhudia washambuliaji wa timu hizo 32 wakishindwa kuivunja
rekodi hiyo ya Ngassa hivyo kumwacha akiendelea kubakia kuwa kinara wa
mabao 6 katika michuano hiyo.
Ngassa aliweka rekodi ya kufunga ‘hat trick’ mbili
katika mechi mbili za hatua ya awali dhidi ya Komorozine de Domoni ya
Comoro ambayo Yanga waliipata ushindi wa jumla ya mabao 12-2. Ngassa
alifunga mabao matatu katika mechi ya kwanza Jijini Dar es Salaam ambayo
Yanga ilishinda mabao 7-0, kabla ya kufanya hivyo tena mjini
Mitsamiouli, Comoro wiki moja baadaye Yanga ilipopata ushindi wa mabao
5-2.
Kwa sasa Ngassa anafuatiwa na washambuliaji
Mouhcine Iajour wa Raja Casablanca ya Morocco na Lamine Diawara wa Stade
Malien ya Mali waliofunga hat trick moja kila mmoja.
Kingston Nkhatha wa Kaizer Chief pia ana mabao matatu aliyofunga katika mechi mbili tofauti.
Endapo Ngassa atafanikiwa kupata mabao mengine na
kuchukua tuzo hiyo ya ufungaji bora wa ligi hiyo, atakua mchezaji wa
kwanza kuweka rekodi hiyo katika historia ya soka la Tanzania.