Maandamano ya kuipinga Urusi, Ukraine.
Kundi la
mataifa saba yaliyostawi zaidi kiviwanda almaarufu kama G7 limelaani
vikali hatua za kijeshi zilizochukuliwa na Urusi nchini Ukraine-viongozi
kundi hilo wakitaja hatua ya Urusi kama ukiukaji wa uhuru wa Ukraine.
Katika
taarifa ya pamoja iliyotiwa pia saini na Umoja wa Ulaya EU-Urusi
imetakiwa kushughulia wasiwasi wake kuihusu Ukraini kupitia mashauri au
upatanishi.
Kundi
hilo la mataifa saba tajiri zaidi duniani maarufu kama G-Seven limesema
kuwa linachukuwa uamuzi wa kuahirisha matayarisho ya kongamano ambalo
lingefanyika nchini Urusi mwezi juni mwaka huu kutokana na vitendo vya
Moscow. Taarifa hiyo inakuja wakati vikosi vya Urusi vikiimarisha
uthibiti katika rasi ya crimea ambapo Urusi inasema kuwa inalinda raia
wake baada ya serikali kupinduliwa mjini Kiev.
Mbunge
mashuhuri wa Urusi - Vyacheslav Nikonov, ameimabia BBC kwamba Urusi
imejiandaa kwenda vitani kulinda maslahi yake nchini Ukraine na hususan
katika mji wa Sevastopol.
"Ukraine
ilialikwa kujiunga na Nato na hii ina maana kuwa marekani, au vituo
vyake vya kijeshi vitawekwa nchini Ukraine. Urusi itafanya lolote,
itahatarisha kuingia vita kuzuia hilo kutokea. Ni kuhusu kituo cha
kijeshi, ni kuhusu mustakabal wa Urusi, mustakabal wa Ukraine. Sidhani
kama mataifa ya magharibi yanaelewa kwamba Ukraine ni mahali ambapo
Urusi ilizaliwa," amesema Nikonov.
Awali
serikali ya mpito ya Ukraine iliishutumu Urusi kwa kutangaza vita na
kuwaamuru wanajeshi wake kuwa tayari kwa makabiliano.Shirika la kujihami
kwa mataifa ya Magharibi NATO limetowa wito kwa Urusi kuwaondoa
wanajeshi wake nchini Ukrainena kuzitaka pande zote kusuluhisha mgogoro
huo kwa njia ya amani. Taarifa hiyo imetolewa baada ya mkutano wa
dharura wa mabalozi wa NATO mjini Brussels kujadili mgogoro huo. Katibu
mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen, amesema kuwa huenda wachunguzi wa
umoja wa mataifa wakatumwa kusaidia kusuluhisha hali ya mambo.
"Tunatoa
wito kwa urusi kuheshimu ahadi zake za kimataifa, kuondoa vikosi vyake
na kujiepusha na uvamizi katika maeneo mengine nchini Ukraine. Tunatowa
wito kwa pande zote kufuata njia ya amani katika kusuluhisha mgogoro huo
kupitia mazungumzo, kupitia wachunguzi wa kimataifa chini ya mwavuli wa
umoja wa baraza la usalama la umoja wa mataifa au shirika la
ushirikiano wa kiusalama ulaya OSCE,'' amesema bwana Rasmussen.
Waziri wa
mashauri ya nchi za kigeni wa marekani , John Kerry, anatarajiwa kuzuru
Kiev hapo kesho jumanne kuiunga mkono serikali mpya ya Ukraine.
Haya
yanajiri wakati mkuu wa jeshi la wanamaji wa Ukraine, Denis Berezovsky,
akipokonywa madaraka yake baada ya kusema hadharani kwamba anaunga mkono
serikali mpya ya Jimbo la Crimea ambayo inaunga mkono Urusi.
Serikali ya Kiev imesema kuwa inamfanyia uchunguzi kwa nia ya kumfungulia mashtaka ya uhaini.
Chanzo, bbcswahili