SHETANI bado anazidi kuwasakama Wakristo duniani. Hii ni baada ya
mkazi wa Kijiji cha Alvaro Thesiss, Santa Catarina nchini Brazil, Mtume
Inri Cristo (66) mwanzilishi wa Kanisa la Waraka Mweusi (Suprema Ordem
Universal da SantÃssima Trindade ‘Soust’), miaka 35 iliyopita
kujitangaza kuwa yeye ni Yesu Kristo amerudi kuja kuwaokoa wanadamu
baada ya kusubiriwa kwa miaka mingi.
Cristo kwa sasa anaitikisa dunia kwa kuwahubiria maelfu ya watu wa
madhehebu ya Kikristo sehemu mbalimbali duniani huku akijiita Yesu
Kristo wa Nazareti.
MAHUBIRI YAKE YATIKISA
Mei, 2013, Cristo alitua
katika Jiji la Sao Paulo nchini humo na kuwaombea Wakristo, wakiwemo
makahaba. Alipokelewa kwa heshima zote huku akijitangaza kuwa hakuna
atayekuja duniani kuwakomboa wanadamu zaidi yake.
Alihubiri kuwa kwa kila kiumbe mwenye matarajio ya kuingia kwenye ufalme wa mbinguni yeye ndiye njia ya kweli na uzima.
YESU FEKI AKUTANA NA MAGUMU
Septemba, 2013, mzee
huyo alitua kwenye Jiji la Rio de Jeneiro kwa lengo hilohilo lakini
alijikuta akishambuliwa vikali huku Wakristo wa jiji hilo wakimtupia
lawama kuwa ni mhubiri feki aliyevaa ngozi ya kondoo kujipatia kipato
kinyume na utaratibu wa makanisa mengine ya Kikristo nchini Brazil.
AITWA MHUBIRI PUNDA
Akiwa katika harakati zake
za kuwavuta waumini wa makanisa ya Kikristo katika Jiji ya Sao Paulo
wakati wa Sikukuu ya Krismasi, mwaka jana, mhubiri huyo feki
alishambuliwa tena na waumini wa eneo hilo ambao walikusanyika kwenye
mkesha wa sikukuu hiyo.
Baadhi ya waumini walimzomea kwa mahubiri yake huku wakisema hayana
tofauti na punda aliyebebeshwa mzigo mzito na kushindwa kuutua.
Hata hivyo, Yesu feki huyo aliwajibu waumini hao kwamba hawajui
walitendalo kwani yeye ndiye Yesu wa kweli aliyetumwa na Mungu kuja
duniani kuwaokoa wanadamu.
“Mimi sijali maneno yao, wameniita punda, eti mahubiri yangu hayana
tofauti na punda aliyebebeshwa mzigo mzito hivyo hawezi kujinasua siku
zote ataishia kutapatapa, mimi nimetumwa na Mungu,” alisema Cristo.
ANASWA NA KASHFA YA UTAPELI
Akiwa amejiamini
na kujijengea heshima kubwa kwa waumini wake, Januari Mosi mwaka huu,
mhubiri huyo alishambuliwa kwa maneno na watu wasiojulikana kwa
kusambaza nyaraka za wazi zilizokuwa zimeandikwa kuwa yeye ni tapeli
mkubwa kwani anadanganya watu ili kujipatia fedha.
Kitendo hicho kilimpunguzia umaarufu kwani alikuwa ameweka utaratibu
kwa waumini wake kulipa fungu la kumi kwa kila pato, alijiweka zaidi kwa
wafanyabiashara wakubwa nchini Brazil huku akiwaonya kuwa bila yeye
hawawezi kufanikiwa kimaisha.
HISTORIA YAKE KIDUNIA
Cristo aliyezaliwa Machi
22, 1948 mwenye wafuasi wengi katika kanisa lake, amewahi kutembelea
nchi nyingi duniani akieneza uzushi huo kwamba yeye ni Yesu Kristo.
Amewahi kufukuzwa kwenye baadhi ya nchi za Ulaya na Amerika ya Kusini
zikiwemo Uingereza, Venezuela, Peru, Marekani na Ufaransa ambako
alitaka kuanzisha makanisa. Pia ameshawahi kuwekwa ndani mara 40 nchini
mwake kutokana na kujitangaza kuwa yeye ni Yesu na kuvuta watu wengi.
Katika nchi yake, Cristo amefanikiwa kuwafanya waumini wake waishi
pamoja naye kwenye makazi jirani na kanisa lake la Santa Catarina.
Wazazi wa mzee huyo, baba Wilhelm na mama Magdalena Thais ni Wakatoliki wenye asili ya nchini Ujerumani.
Tangu mwaka 1979, Cristo amesafiri zaidi ya nchi 27 duniani kote
akieneza neno lake huku akisema yeye ni Mfalme wa Wayahudi aliyerejea
duniani kwa mara ya pili. Pia husema eneo la kanisa lake ni Yerusalemu
mpya.
MAVAZI YAKE
Mara zote, Cristo huvaa kanzu nyeupe
na viatu vya ‘makubazi’ huku kichwani akiwa na mduara wenye kuashiria
taji la miiba alilovalishwa Yesu wa kweli.
ETI ALIISIKIA SAUTI YA MUNGU
Katika mahojiano
yake na baadhi ya redio nchini humo, mhubiri huyo amekuwa akisema tangu
utotoni mwake alikuwa akiifuata sauti ya Mungu ambayo ilikuwa ikisema:
“Mimi ni Baba yako. Mungu wa Ibrahim, Isaka na Yakobo.”
ANA MPANGO WA KUTEMBELEA AFRIKA
Inasemekana wakati wowote mwaka huu, Cristo atatembelea nchi mbalimbali za Bara la Afrika kwa lengo la kuvuta wafuasi wengi.
Nchi za Zimbabwe, Afrika Kusini, Tanzania, Togo, Mali, Misri, Angola,
Nigeria, Burkina Faso na Zaire zinadaiwa kuwepo kwenye ratiba ya ‘Yesu’
huyo.
VIONGOZI WA DINI NCHINI WAMKEMEA
Gazeti hili lilizungumza na baadhi ya wachungaji na maaskofu wa Tanzania kusikia wanamzungumziaje mhubiri huyo feki.
MCHUNGAJI MTIKILA
Mchungaji wa Kanisa la Full Salvation Church la jijini Dar es Salaam,
Christopher Mtikila alipopigiwa simu na kuulizwa kuhusiana na sakata
hilo, alisema:
“Huyo ni shetani mkubwa, akija Tanzania hatutaki kumwona kwani anakuja kuwavuruga waumini wetu.”
ZAKARIA KAKOBE
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship lenye makao yake
makuu kwenye Jiji la Dar es Salaam, Zakaria Kakobe naye alikuwa na haya
ya kusema:
“Huyo akija Dar anatakiwa tumuombee ili mapepo yamtoke, awe mzima na amsifu Mungu.”
MZEE WA UPAKO
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi nalo la jijini Dar, Lusekelo Antony
‘Mzee wa Upako’ alisema utabiri wa Yesu kuwa nyakati za mwisho wengi
watajitokeza wakidai ni Kristo umetimia.
“Hizi ni nyakati za mwisho kweli. Yesu alisema watatokea manabii
wengi wakisema wao ndiyo Kristo, ndiyo hao sasa. Hataweza kuushinda
utawala wa Mungu aliye hai,” alisema Mzee wa Upako.