MSAFARA
wa timu ya Yanga SC ya Dar es Salaam leo mchana umepata fursa ya
kumtembelea Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Chabaka Kilumnaga kufuatia
mwaliko wa timu pamoja na viongozi katika hafla ya chakula cha mchana
nyumbani kwake eneo la Itsandra Moroni.
Katika
hafla hiyo Balozi Chabaka alishukuru timu ya Yanga kwa kufika nyumbani
kwake na kujumuika katika chakula cha mchana pamoja na maofisa wa
ubalozi waliopo nchini Comoro na Watanzania wengine wanaoishi kwenye
kisiwa hicho cha Ngazija.
Balozi
wa Comoro nchini Tanzania, Dk Ahmed El Balidou na Waziri wa Elimu
nchini Comoro nao pia walikuwepo ambao kwa pamoja waliukaribisha msafara
wa Yanga na kuwaambia wajisikie wapo nyumbani.
“Nawakaribisha
sana hapa Comoro mjisikie kama mpo nyumbani Tanzania, pili
nilifurahishwa na ushindi katika mchezo wa jana ambao niliuhudhuria na
mkaweza kuibuka na ushindi, hiyo ilikuwa inaendeleza sifa nzuri ya Yanga
pamoja na nchi ya Tanzania kwa ujumla,”alisema Chabaka.
Aidha,
Balozi Chabaka alisema anaitakia kila la kheri Yanga katika mchezo wake
unaofuata dhidi ya Al Ahly na kusema timu hiyo ina nafasi nzuri ya
kufanya vizuri na kusonga mbele kwa kuwang'oa vigogo hao wa soka barani
Afrika.
Mkuu
wa msafara wa Yanga SC, Ramadhani Nassib ambaye ni Mjumbe Mteule wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), aliushukuru ubalozi wa kuikaribisha
Yanga nyumbani kwake kwa ajili ya chakula cha mchana na kuwatakia maisha
mema na yenye mafanikio nchini Comoro ambapo ndio kwanza Ubalozi
umeanza miezi mitatu iliyopita.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa Yanga, Seif Ahmed ‘Magari’
alimshukuru Balozi Chabaka kwa jana kuja uwanjani kuipa sapoti timu na
leo kwa kuialika kwa ajili ya chakula cha mchana.
Yanga
itandoka kesho kurejea nchini Tanzania majira ya Saa 6:30 mchana kwa
ndege na itafika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)
Saa 8:00 mchana.
Yanga
jana ilihitimisha vyema Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa kwa
kuichapa Komorozine mabao 5-2, hivyo kufuzu kwa ushindi wa jumla wa
12-2, baada ya wiki iliyopita kushinda 7-0 Dar es Salaam na sasa
itakutana na mabingwa wa Afrika, Al Ahly mwezi ujao.