UNAWEZA ukakataa lakini ndivyo ilivyotokea, ndoa ya mtangazaji mahiri
Bongo, Gardner Gabriel Fikirini Habash ‘Kapteini’ na Mbongo Fleva,
Judith Wambura Mbibo ‘Jide’ iliyofungwa miaka 9 iliyopita inadaiwa
kuingia kidudu kufuatia mke huyo kuomba aandikiwe talaka, ni Ijumaa
Wikienda pekee lenye uthubutu wa kuripoti mkasa wote.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha kuaminika, Jide au Lady Jaydee
alifikia uamuzi huo baada ya Gardner kupata kazi ya kutangazia redio
moja nchini Kenya.
HABARI KAMILI
Mnyetishaji wa kisanga hiki,
aliliambia Ijumaa Wikienda kuwa mara baada ya mume huyo kupata mchongo
mzima alirudi nyumbani akiwa na furaha na kumwambia mkewe kuhusu bahati
hiyo.
“Baada ya Gardner kupata mchongo wote wa kazi alikwenda mbio nyumbani kwake Kimara (Dar) ili akamwambie mkewe.
“Pia katika safari ya kwenda Kenya kupiga mzigo ilikuwa aende na
mkewe huyo kwa sababu lilikuwa suala la kuhamisha makazi yao Tanzania,”
kilisema chanzo hicho.
JIDE AHAMAKI
Chanzo kikatoboa kwamba Gardner alipofika nyumbani kwake na kumweleza mkewe, alikumbana na kitu ambacho hakukitarajia.
“Komando (Jide) alihamaki na kumjia juu akisema yeye hawezi kuondoka
Tanzania kwenda kuishi Kenya, kama Gardner analiona jambo hilo ni heri
kwake, amuandikie talaka yake na kuachana ili kila mmoja achukue hamsini
zake,” chanzo kilizidi kuporomosha maneno.
KWA NINI JIDE HAKUPENDA?
Habari zilizidi
kuanikwa kwamba Jide au Binti Machozi alifikia uamuzi huo baada ya
kugundua kuwa kitendo cha kwenda kuishi Kenya kitaua bendi yake ya
Machozi na sehemu ya biashara ya Nyumbani Lounge iliyopo Ada-Estate,
Kinondoni, Dar.
MBAYA ZAIDI
Taarifa zikazidi kumiminika kwamba,
mbali na Jide au Anakonda kuhofia biashara zake kufa, lakini pia
hakupenda Gardner aondoke hata peke yake kwa sababu yeye ndiye meneja wa
miradi hiyo miwili.
“Mimi nilipopata habari hizo nilikutana na Jide nikamuuliza,
akanijibu ameamua iwe hivyo tu, kikubwa mumewe (Gardner) aamue moja kati
ya hayo mawili kwani yeye ana haki akiwa kama mkewe wa ndoa,” kilisema
chanzo kikimkariri Jide.
GARDNER AISHIWA NGUVU
Kufuatia majibu ya mkewe,
taarifa zinasema mtangazaji huyo ambaye alishawahi kupiga mzigo kwenye
kituo cha Radio Clouds FM cha jijini Dar alijikuta akiishiwa nguvu na
kuachana na dili hilo mara moja.
“Gardner alisalimu amri kwa mkewe, akaamua kuachana na dili la kwenda
kutangaza Kenya. Lakini alifikiri sana akasema ni kweli kuhamia Kenya
kungeua miradi yao ya Tanzania maana ingekosa msimamizi wa kuaminika,”
chanzo kiliweka wazi.
KAMA ANGEKWENDA KENYA
Siri hiyo iliyovujia
mikononi mwa Ijumaa Wikienda haikuishia hapo, ilizidi kuanikwa kwamba
kama Kapteini angekwenda Kenya na kuanza kazi, ilikuwa alipwe mshahara
wa shilingi za Kenya laki 3 kwa mwezi (kama milioni 6 za Tanzania).
NAFASI YAKE BADO IPO
Mpashaji wetu alisema kwamba nafasi ya Gardner kwenye kituo hicho cha
redio ambacho hakikutajwa, bado ipo lakini tamko la Jide nalo li hai,
kwa vile hakubatilisha, endapo mumewe atataka kwenda hata kesho
(Jumanne) aandike talaka.
WIKIENDA NA GARDNER
Baada ya kunyetishiwa
taarifa nzima, juzi gazeti hili lilimsaka Gardner. Kwa njia ya simu
lilimkosa, likamfuata Nyumbani Lounge. Lilipomkuta lilimsimulia kisanga
chote cha ndoa yake kutikiswa na kitendo cha yeye kupata kazi Kenya
ambapo alijibu hivi:
“Ndoa ni nzuri, ni kweli ilikuwa niende Kenya, nilipata kazi kule
lakini kama familia ilikuwa lazima tukae na kupanga, mwenzangu
hakuafiki.”
Wikienda: “Ni kweli shemeji ameomba uchague mawili, umwandikike talaka au uende Kenya?”
Gardner: “Ndiyo maana nimesema ndoa nzuri, lazima makubaliano yawepo,
mke anaweza kuonesha msimamo wake na mume kama utakaa chini na
kuufikiria ukapata jibu unakubaliana na mke wako wala hakuna ubaya.”
Wikienda: “Kule mshahara wako ungekuwa shilingi ngapi?”
Gardner: “Hiyo sasa ni siri ya makubaliano.”
Wikienda: “Kwa nini usiamue kwenda tu?”
Gardner: “Nimekwambia ndoa nzuri.”
JIDE BIZE
Juhudi za kumpata Jide ziligonga
mwamba baada ya muda wote kuwa bize na shoo ya kukata na shoka aliyokuwa
akiifanya siku hiyo kwenye ukumbi huo akikimbiza na nyimbo zake kali za
zamani na hizi mbili zilizogeuka nyimbo za taifa, Joto Hasira na
Yahaya.
RAFIKI WA GADNER AMCHAMBUA JIDE
Rafiki wa karibu
na Gardner (jina tunalo) ambaye alisikia mahojiano ya mtangazaji huyo
na Ijumaa Wikienda, alisubiri jamaa aondoke ambapo alianza kumchambua
Jide.
“Nataka kuwaambia kitu, Jide ni mwanamke jasiri sana. Ana
msimamo na anaposhikilia msimamo wake hatengui hasa kama atabaini kuwa
yupo sahihi.
“Ni kweli jamaa (Gardner) alipata kazi Kenya tena mshahara mzuri tu,
lakini mama (Jide) akaweka ngumu hakuna kwenda,” alisema rafiki huyo.