LAZIMA utokwe machozi! Grace John mkazi wa Mzumbe, Mvomero mkoani
Morogoro yupo kwenye wakati mgumu kutokana na maradhi ya ajabu
yanayomsumbua mwanaye Honolina Christian Mkude (11).
Honolina anasumbuliwa na ugonjwa wa kuota nyama sehemu za mwili wake
zinazofanana na pembe za mnyama, ugonjwa ambao unamtesa tangu kuzaliwa
kwake.
ILIKUWAJE?
Akisimulia kisa kizima, mama mzazi wa Honolina, Bi. Grace, anasema tangu amemzaa mwanaye huyo ni mitihani baada ya mitihani.
Mazungumzo hayo yalifanyika hivi karibuni katika kituo cha mabasi ya
mikoani, Msamvu, mjini hapa wakati mama huyo na mwanaye wakihangaikia
kuchangisha fedha za usafiri wa kwenda Moshi kutafuta tiba zaidi katika
Hospitali ya Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC).
“Ndugu mwandishi, kwa kweli sijui hatima ya mwanangu. Nilimzaa akiwa
ameota nywele sehemu zote za mwili wake, hadi usoni. Mimi na mume wangu
tulishangaa, lakini tuliendelea na matibabu katika hospitali mbalimbali
maana baadaye alianza kupatwa na uvimbe.
MTIHANI MWINGINE
“Jamani ndugu yangu... Mungu ana
mitihani yake. Mume wangu (Christian Mkude) ambaye ndiye alikuwa
tegemeo pekee kwetu, alifariki mwaka 2007 kwa ajali ya gari, wakati
akisaka fedha za matibabu ya mwanetu.
“Kifo chake, kwangu kimekuwa pigo mujalabu. Sina pa kukimbilia na
hivi juzi tu tulikuwa tumelazwa Hospitali ya Mkoa (Morogoro) na hapo
tumepewa barua ya kwenda KCMC kwa matibabu zaidi.
“Hivi unavyoniona
nachangisha fedha ili nipate angalau nauli za kutufikisha kwanza
hospitalini. Nimechanganyikiwa kabisa,” alisema Bi. Grace kwa majonzi
na kuongeza:
“Wakati tatizo la mwanangu linaanza sikutegemea kama siku moja
angekuja kuwa hivi. Zilianza kuota nywele mwili mzima, baadaye vidonda
vikaanza kumtoka na sasa hali imebadilika na kuota nyama hizi kubwa kama
mapembe kama unavyoona.”
SAUTI YA BI. GRACE KUTOKA MOSHI
Misaada ya fedha
kidogo alizopata kwa wasamaria wema waliomuona Msamvu, ulimsaidia mama
huyo kusafiri hadi Moshi na kufika katika Hospitali ya KCMC.
Akizungumza
kwa njia ya simu kutoka Moshi, Bi. Grace alisema: “Nawashukuru
waliniosaidia, tumefika salama na mwanangu hapa KCMC, ndiyo tumeanza
taratibu za matibabu.”
BADO ANAHITAJI MSAADA
“Madaktari wametupa moyo,
wamesema watajaribu kumsaidia mwanangu. Watamtoa hizo nyama ila kwa
sababu kutabaki na mashimo lazima wapandikize nyama nyingine.
“Tumeshakubaliana
kuwa mimi ndiye nitakayekatwa sehemu ya nyama kutoka kwenye makalio
yangu kwa ajili ya kumsaidia mwanangu,” alisema Bi. Grace, kilio
kikisikika kwenye simu.
Akaongeza: “Wameshachukua nyama za mwanangu na kwenda kupima na
baadaye watachukua zangu ili kuona kama zinaendana, upasuaji ufanyike.
Gharama kwa ajili ya matibabu hayo wamesema ni shilingi 400,000 na mimi
sina uwezo.
“Watanzania wenzangu, naombeni mnisaidie ili niweze
kuondokana na hili tatizo. Mimi ni mjane na sina kazi ya kueleweka,
napigania uhai wa mwanangu. Naombeni msaada wenu,” alisemaSHIRIKI BARAKA
Kumsaidia mhitaji wa kweli
huongeza baraka katika kipato, vitabu vitakatifu vinaeleza wazi. Ndugu
wasomaji wetu wapenzi, kwa yeyote atakayeguswa na mateso ya familia hii,
anaweza kumsaidia chochote mama huyo kupitia simu zake namba 0719
749542 (Tigopesa) na 0762 425973 (M - pesa).
