![]() |
| Basi la Taqwa. |
Dereva wa basi la kampuni ya Taqwa, Adam
Ibrahim (50) amekufa papo hapo huku abiria kumi wakijeruhiwa baada ya
basi alilokuwa anaendesha kutoka Dar es Salaam kwenda Bujumbura, Burundi
kugongana na lori katika kitongoji cha Ngonho, Kata ya Miguwa wilayani
Nzega.
Ajali hiyo imethibitishwa na Mkuu wa Wilaya
ya Nzega, Bitun Msangi aliyesema ilitokea juzi saa 2 usiku. Amelitaja
basi hilo kuwa ni lenye namba T 532 BYJ lililogongana na lori aina ya
Scania lenye namba za usajili T 984 AGK.
Alisema dereva wa Taqwa alikuwa katika
mwendo kasi akitaka kulipita gari aina ya Mitsubishi Fuso lililolokuwa
mbele yake na aliongeza mwenda ili alipite, alikutana na lori hilo
lililokuwa linaendeshwa na Khalfani Hussein aliyejeruhiwa vibaya na
kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Nkinga wilayani Igunga.
Msangi aliwataja majeruhi wengine kuwa ni
Aziza Nassoro na Tatu Shabani ambao ni raia wa Burundi, Marieta Petro,
mkazi wa Singida, Mwanakaombo Tau Mkazi wa Nzega, Tau Omary mwanafunzi
wa chekechea mkazi wa Nzega, Khadija Rashidi mkazi wa Dar es Salaam,
Hamad Ally ambaye ni fundi wa basi la Taqwa na Richard Mtaru, mkazi wa
Moshi ambaye ni dereva msaidizi wa basi hilo.
Kutokana na ajali hiyo, Msangi amewataka
madereva kuzingatia na kutii sheria barabarani ili kupunguza ajali
zinazoweza kuepukika.
Majeruhi hao wakizungumza kwa nyakati
tofauti katika hospitali ya wilaya ya Nzega walisema kuwa chanzo cha
ajali hiyo ni mwendo kasi wa basi hilo.
Mganga Mkuu Mfawidhi wa wilaya, Emmanuel
Mihayo alisema afya za majeruhi hao zinaendelea vizuri huku wengine
wakitarajiwa kupewa ruhusa tayari kwa kuendelea na safari zao.
Ajali hiyo ni moja ya ajali za barabarani
ziliripotiwa wiki hii, zikiwemo mbili zilizoua watu 26 huko Singida na
Lindi siku ya Jumatatu.
Ajali ya kwanza iliyoua watu 13 papo hapo
na mmoja kujeruhiwa, ilitokea baada ya gari dogo la abiria aina ya
Toyota Noah walilokuwa wakisafiria, kugongana uso kwa uso na lori la
mizigo eneo la Isuna, barabara kuu ya Singida-Dodoma.
Ya pili ni iliyoua watu 13 na kujeruhi
wengine 25 baada ya basi la Al Hamdullilah walilokuwa wakisafiria kutoka
Dar es Salaam kwenda Mtwara, kuacha njia na kupinduka mtaroni saa 7.30
mchana.
