Monday, 30 December 2013

TUNAMALIZA MWAKA, TUBADILIKE MWAKANI

Mambo vipi maanko, naamini mko poa.
Mwaka unamalizika siku chache zijazo, panapo majaaliwa, tutakapokutana tena hapa Jumamosi ijayo, utakuwa ni mwaka mwingine. Tuna mengi ya kujiuliza, ya kujifunza na hata ya kufikiria.

Tokea tulipoanza kukutana hapa, tumezungumza mambo mengi sana, tumekumbushana, tumefundishana na hata kusifiana. Binafsi, ninaamini nyinyi mlikuwa na mambo mengi zaidi kuliko mimi, lakini kwa bahati mbaya mlishindwa kupata fursa ya kunifikishia yaliyomo vichwani mwenu.
Wengi wenu hata hivyo, mlipata nafasi ya kuchangia nami mawazo, ninafurahi kwamba licha ya wanafunzi, pia baadhi ya walimu nao walishiriki kuchangia maoni yao. Jambo moja la msingi nililojifunza ni kwamba tunayo nafasi ya kubadilika na kuwa bora zaidi.
Mwaka unaokuja, uwe wa kujaribu kubadilika, kwa kadiri tunavyoweza. Kila mmoja aiweke nafsi yake katika kutaka kuwa bora, kitaaluma, kitabia na kwa wenye vipaji maalum, kujiendeleza zaidi.
Kwa mfano, tulizungumza kuhusu tabia ya wanafunzi kujihusisha kimapenzi baina yao. Tulisema siyo tabia nzuri kwani mara nyingi inasababisha kupoteza muda mwingi kufikiria ngono badala ya masomo.
Tulizungumza pia kuhusu walimu nao kutumia nafasi yao kuwalazimisha mapenzi wanafunzi. Ni tumaini la kijiwe hiki kwamba na wao, watajitahidi kubadilika ili waachane na tabia hiyo isiyo njema.
Somo la ngono lilikuwa pana sana, kwani liliwahusu hadi wanafunzi wenyewe, kwamba wakati mwingine ni wao ndiyo wanaowahamasisha waalimu ili washiriki nao mapenzi.
Kitu kikubwa nilichojifunza kupitia maoni yenu mbalimbali, ni kwamba suala la uhusiano wa kimapenzi mashuleni ni tatizo kubwa sana, iwe kwa kutishana au kwa mapenzi tu. Ni nadra sana kwa binti kupenya hadi anamaliza angalau kidato cha nne bila kuvunja amri ya sita!
Lakini kama nilivyosema, hakuna kinachoshindikana. Tukiamua, tunaweza kuwa bora zaidi kuliko jana.
Nimekuwa nikisisitiza mara kwa mara, kwamba nafasi yetu ya kusoma ni moja tu, tukiipoteza hivi sasa kwa sababu zozote zile, baadaye tutakuja kujuta, kama ambavyo mimi anko wenu ninavyojuta kila siku.
Kama ningejitambua na uwezo wa kiakili niliokuwa nao, hakika leo ningekuwa nakula bata kweli kweli, kwa sababu asikudanganye mtu bwana, elimu haiangushi. Yaani ukiwa na shule ya kutosha, una uhakika na maisha.
Kwa maana hiyo, jaribuni sana kuutumia mwaka ujao kama ambao unaweza kubadili maisha yenu. Kama ulikuwa mtoro wa vipindi, ulikuwa mvuta bangi, mpenda ngono, jeuri kwa walimu, mpiga kelele darasani, jaribu kubadilika, hata angalau kwa asilimia 50 tu.

Enzi zetu tukisoma, tulikuwa tunawaita watu wanaotushauri kusoma kama wanoko, eti tukiwabeza kama elimu ni mali mbona wao hawakusoma. Kumbe nimekuja kugundua kuwa tunatambua thamani ya shule baada ya kuwa tumeshaikosa na muda hauruhusu tena.
Labda nyinyi hamjui, lakini niwaambie kuwa siku hizi watu wazima wanaenda shule, wamekuja kugundua thamani yake ukubwani. Mimi mwenyewe najiandaa kwenda Open University, nikaongeze elimu.
Sasa fikiria mwenyewe, kama mimi kwa umri wangu huu bado naamini elimu inaweza kunisaidia maishani, sembuse wewe kijana mdogo ambaye hata miaka ishirini bado? Au una 30?
Huku mtaani mambo ni magumu kweli kweli na kadiri miaka inavyokwenda, yawezekana yatakuwa magumu zaidi, hasa kwa wasio na shule, lakini kwa wenye shule zao, mambo yatakuwa rahisi kweli, maana wawekezaji wengi wanakuja, miradi mingi mikubwa inakuja na fursa zaidi zinakuja katika soko kubwa la ajira kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Watatafutwa vijana wenye elimu nzuri na nina uhakika kama ukiamua kuufanya mwaka ujao kuwa wa mabadiliko kwako, una uhakika na ajira ya kukulipa mamilioni kila mwezi. Happy New Year!.